Dar es Salaam. Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeita wawekezaji kuwekeza kwenye hatifungani ya muda mrefu ikiahidi riba ya asilimia 15.49 kila mwaka.
Taarifa iliyotolewa na BoT Desemba 11, 2024 katika tovuti yake ilionyesha Serikali inahitaji kukusanya Sh156 bilioni kwenye mnada utakaofanyika Desemba 18, 2024.
“Mnada huo utakaofanywa kupitia Benki Kuu ya Tanzania unatarajia kukusanya Sh156 bilioni kwa ajili ya zabuni shindani na ziada ya Sh34 milioni itatengwa kwa wazabuni wasio na ushindani.
“Hatifungani hizo ambazo zilitolewa kwa mara ya kwanza Mei 23, 2019, tarehe yake ya kuiva itakuwa Mei 22, 2039. Wawekezaji wanatakiwa kuwasilisha zabuni mtandaoni kupitia taasisi washiriki (CDPs) kabla ya saa 11:00 asubuhi katika tarehe ya mnada,” imesema taarifa hiyo.
BoT imesema kiwango cha chini cha uwekezaji katika hatifungani hizo ni Sh1 milioni.
Pia, mnada huo utakaoanza Desemba 18, BoT imesema utasajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) sambamba na ule wa pili utakaoanza Desemba 20, 2024.
Akizungumzia hatifungani hizo, mchumi Mack Patrick amesema zitasaidia kuvutia wawekezaji wa muda mrefu na zitaimarisha masoko ya fedha ya Tanzania.
“Mpango huu utahakikisha upatikanaji wa soko na ukwasi, pia kuvutia wawekezaji wa muda mrefu na kuimarisha sekta ya fedha nchini. Pia itakuza masoko ya fedha na hatimaye ukuaji wa uchumi,” amesema Patrick.