‘SIMBA ndo zetu… Simba Ubaya Ubwela…Simba ndo zetu…’ Ni baadhi ya nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na mashabiki wa Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakifurahia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, huku Kibu Denis akimaliza ukame wa mabao wa siku 84 kwa kukwamisha mabao yote.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi sita baada ya mechi tatu za Kundi A katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuipumulia CS Constantine ya Algeria ambayo ilikuwa uwanjani usiku wa jana kupepetana na Bravos do Maquis ya Angola, huku ikiendeleza rekodi nzuri ya kutumia uwanja wa nyumbani.
Mechi ya jana ilikuwa ya 36 kwa Simba kucheza nyumbani katika michuano ya aina yote ya CAF tangu mwaka 2018, huku ikishinda 26, ikipoteza mitatu na kutoka sare mara saba, lakini ikivuna jumla ya mabao 75 na kufungwa 20 tu na Wekundu hao sasa wamebakiwa na mechi moja tu ya nyumbani na mbili za ugenini.
Katika mchezo wa jana Kocha Fadlu David aliwaanzisha viungo wanne, akiwamo Debora Mavambo, Awesu Awesu, Fabrice Ngoma na Jean Ahoua, huku Abdulrazak Hamza mahali alitumika Chamou Karaboue aliyeingizwa kipindi cha pili kumpokea Fondoh Che Malone, ambaye jana alikuwa na siku mbaya kazi.
Katika mchezo huo uliokuwa wa tatu kwa timu, Simba ilishtukizwa na wageni kwa kufungwa bao la mapema la dakika ya tatu tu tangu kuanza kwa pambano hilo baada ya beki Fondoh Che Malone kuzembeakuokoa mpira na kumruhusu mshambuliaji Hazem Hassen kufunga kirahisi.
Hata hivyo mashabiki wa Simba hawakukata tamaa waliwapigia wachezaji makofi yaliyowatia nguvu nyota wa timu hiyo na kufanya bao hilo lirudishwe dakika ya saba kupitia kichwa cha Kibu Denis akipokea mpira wa adhabu ndogo ya Charles Ahoua.
Hilo lilikuwa bao la kwanza kwa Kibu tangu alipofunga mara ya mwisho katika mechi za raundi ya pili wakati Simba ikitambia Al Ahli Tripoli ya Libya kwa mabao 3-1 mchezo uliopigwa Septemba 22 mwaka huu, ambalo pia lilisaidia kuwarudisha Wekundu katika mstari na kutawala mchezo huo kwa dakika 45 za kwanza.
Simba ingejilaumu kama isingetoka na ushindi kwani ilitengenezxa nafasi nyingi lakini zikapotezwa na washambuliaji wa timu hiyo akiwamo Leonel Ateba aliyeanza kikosi cha kwanza na hata Steven Mukwala aliyekuja kumpokea kipindi cha pili, mbali na yale ya Jean Ahoua na Kibu Denis walioshindwa kutumia krosi tamu za Shomary Kapombe aliyeng’ara mchezo wa jana.
Haikuwa siku nzuri kwa Che Malone baada ya kufanya makosa matatu hatarishi akipoteza mpira maeneo hatarishi ambayo yalibaki kidogo kuigharimu tena timu yake.
Baada ya makosa hayo kocha Fadlu Davids ilimtoa beki huyo ambaye alionyesha kujiamini akatolewa nafasi yake ikienda kwa Karaboue Chamou ambaye angalau ukuta wa timu hiyo ukaonyesha kutulia.
Timu zote zilifanya mabadiliko matano kila mmoja, lakini Simba ikiingiza wachezaji wengi wa kutengeneza nafasi na kutuliza kwenye ulinzi hawakuwa na jipya katika kubadilisha matokeo.
Hali hiyo pia ikawa kwa CS Sfaxien ambao waliingiza wachezaji wa kutunza mpira wakitafuta angalau pointi moja, kabla ya Kibu kuwatibulia dakika za jionii, zilizoifanya wababe hao wa Tunisia wenye rekodi ya kutwaa mara mbili Kombe la Shirikish0 (3) kupoteza mchezo wa tatu mfululizo na kuendelea kusalia mkiani.
Mashabiki wa Simba hawakufurashwa wakati muda ukielekea ukingoni hasa baada ya kuongeza dakika saba za nyongeza, wakichukizwa na jinsi timu hiyo ikipoteza nafasi za wazi na kuwapa presha zaidi mastaa kabla ya Kibu kuwatuliza kwa kufunga bao dakika ya 90’+9′ lililozua tafrani kutoka kwa wageni.
Wakati mashabiki wa Simba wakiamini mchezo huo utamalizika kwa sare, Mkandaji alifunga bao la pili na la ushindi kwa kichwa akimalizia krosi ndefu kutoka kwa Yusuf Kagoma aliyeingia kumpokea Debora Mavambo na kuifanya Simba kuibuka na mabao 2-1 na kuzoa pointi zote tatu Kwa Mkapa.
Wakati Simba ikishangilia bao hilo humu mwamuzi AndofetraAroniania kutoka Madagascar akakutana na vurugu kubwa kutoka kwa wachezaji na baadhi ya maafisa wa benchi la ufundi la CS Sfaxien wakimsukuma mwamuzi huyo
Vurugu hizo zikiendelea kuimarika ambapo hata baada ya walinzi maalum wa uwanjani ‘Steward’ kuingia kuwaokoa waamuzi hao nao wakakutana na kipigo kutoka kwa wachezaji na viongozi hao.
Vurugu hizo zikachukua sura ya tatu kwa mashabiki wachache wa Sfaxien majukwani kuanzisha vurugu na kuwafanya mashabiki baadhi wa Simba nao kuanza kuwajibu huku viti vikivunjwa.
Hata hivyo hali ikatulia baada ya walinzi kufanya kazi nzuri kuwatuliza mashabiki hao pamoja na wachezaji wao wakiwazingira katikati ya uwanja huku mashabiki wa Simba wakiendelea kufurahia ushindi majukwani.
SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala/Nouma, Hamza, Che Malone/Karaboue, Mavambo/Kagoma, Awesu, Ngoma, Ateba/ Mukwala, Ahoua/Mutale na Kibu.
SFAXIEN:Dahmen, Derbali, Baccar, Nasraoui/Kouame, Layouni, Conte, Pedro, Sekkouhi/Traore, Habbassi/Hamid, Cristo/Becha na Haj Hassen/Haboubi