TUONGEE KIUME: Ni rahisi kununuliwa pombe kuliko chakula

Jamaa mmoja alikuwa na shida ya shilingi elfu hamsini. Akachukua simu akampigia rafiki yake na kumuomba amkopeshe. Rafiki yake akajibu kwamba, hana. Jamaa akaona isiwe kesi, kama elfu hamsini ni kubwa, basi hata elfu ishirini. Rafiki yake akamwambia, hata hiyo sina, hali yangu mbaya.

Baadae jamaa akapigiwa simu na yule rafiki yake.
“Uko wapi?” jamaa akaulizwa.
“Niko nyumbani” jamaa akajibu.
“Mimi niko Chobingo Bar. Njoo chapchap kama vipi,” rafiki yake akamuita.

Hapa Chobingo Bar ndipo wanapokunywaga pombe kila siku. Lakini kwa sababu mchana jamaa alimuomba rafiki yake mkopo wa elfu hamsini, kuitwa Chobingo kulimuweka njiapanda, hajui rafiki yake anamuita ili akanywe pombe au ili akampe ile elfu hamsini.

Haraka jamaa anagundua hawezi kupata majibu akiwa nyumbani. Anafunga safari mpaka Chobingo Bar, anafika anamkuta rafiki yake na bila kucheleweshwa jamaa akaanza kununuliwa pombe.

Anakunywa pombe, anakunywa pombe, anakunywa pombe mpaka basi. Halafu usiku kabisa wanaagana na rafiki yake wakiwa mbwii. Rafiki yake anamuacha mikono mitupu, hata senti tano hampi. Ndiyo sasa jamaa anapata jibu, kumbe aliitwa kwa ajili ya kunywa pombe na wala siyo kujaribu kumpatia msaada wa tatizo lake.

Jamaa akabaki anajiuliza hiyo pesa aliyotumia kumnunulia pombe si bora angempa yeye amalize shida yake iliyokuwa inamsumbua.

Nimesimulia stori hii kwa sababu wanaume wengi tutakutana nayo kipindi cha mwisho wa mwaka. Tutakuwa na shida, tutapigia rafiki zetu, lakini kuna uwezekano wakashindwa kutusaidia, lakini wakawa na pesa ya kutununulia pombe. Na ukikutana nayo unaweza ukamlaumu rafiki kwa kuwa mtu wa ina hiyo.

Sasa sikia, kwanza mwanaume kuwaza hivyo ni kuyumba. Kwa nini? Kwa sababu pesa ya mwenzako hutakiwi kuipangia matumizi. Hata kama ni kweli shida yako ilikuwa ni kubwa na msaada wake ungekuwa wa thamani sana, lakini jinsi mtu mwingine anavyotumia pesa zake haitakiwi kukuhusu. Haijalishi ni ndugu yako wa damu au rafiki.

Lakini pia unadhani ni kwa nini waswahili walisema mlevi yuko radhi akununulie pombe unywe mpaka ushindwe kutembea, lakini sio kununulia chakula hata kama una njaa ya kufa. Hiyo ndiyo kawaida ya walevi. Jambo ambalo linazua swali la kwa nini iko hivyo?

Ukweli ni kwamba, mlevi mwenzako anapokuita kukunulia hufanya hivyo siyo kwa sababu anakupenda, na wala kukununulia kwake pombe siyo zoezi analolifanya kwa ajili yako, bali anajifanyia yeye.

Mlevi mwenzako anakununulia pombe kwa sababu anapenda kampani yako. Na anagundua ili aipate, inabidi ailipie. Hawezi kuilipia kwa kukulipa pesa mkononi kama yuko kwa mangi ananunua sukari, badala yake anakulipa kwa kukulipia kile unachokipenda, kile kinachowakutanisha, pombe.

Kwa lugha nyepesi, hatilii maanani sana kuhusu maisha yako. Cha muhimu kwake ni kampani yako. Ni namna gani pombe zinanoga akiwa na wewe. Tujiandae kukutana na matukio mengi kama haya kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, kipindi cha sherehe, sikukuu na kutumia pesa.

Related Posts