Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema katika uongozi wake atasukuma kwa kadri awezavyo kuhakikisha kila mkandarasi anayedai analipwa.
Pia ameelekeza ujenzi wa kila barabara hasa katika Jiji la Dar es Salaam uende sambamba na uwekaji wa taa za barabarani.
Ulega amesema hayo leo Jumapili Desemba 15, 2024 alipofanya ziara kutembelea ujenzi awamu ya tatu ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na upanuzi wa Barabara ya Morogoro kutoka Ubungo – Kimara.
Ulega amesema: “Katika kipindi changu niwahakikishie nitasukuma kwa kiwango cha juu kuhakikisha hakuna haki ya makandarasi inapotea,” amesema.
Amesema utekelezaji wa hilo utawazingatia makandarasi wazawa ili waimarike.
Akiwa Gongo la Mboto kukagua mradi wa BRT, Ulega amesema hatamvumilia mkandarasi atakayezembea kutekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba.
Kwa sababu kazi zinatolewa kwa masharti ya mkataba, amesema atatumia masharti hayo kuwachukulia hatua watakaozembea akiahidi atahakikisha hawapati nafasi ya kufanya tena kazi nchini.
Kwa wanaofanya vizuri, amesema atawapongeza na kuhakikisha wanaendelea kushirikiana katika kazi zijazo. “Sitakuwa na subira wala uvumilivu kwa mkandarasi mzembe na anayefanya vizuri tutaendelea kumpa kazi na kumpongeza,” amesema.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya BRT ya Nyerere amesema umefikia asilimia 70 kama ilivyo katika mkataba.
Amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika Machi, 2025 akieleza mkandarasi anakwenda vema.
Kwa mujibu wa Ulega, barabara hiyo inatumiwa na wengi ni vema wakati wa ujenzi inapowezekana kutoa nafasi ya watumiaji wengine ifanywe hivyo.
“Pale mnapoona inawezekana mtoe njia ili watu wapite mfanye hivyo ili watu wapite na waendelee na shughuli nyingine,” amesema.
Amesema ujenzi wa kila barabara jijini Dar es Salaam uende sambamba na uwekwaji wa taa za barabarani.
“Nisingependa kuona katika mji barabara zinakuwa na giza na kasi ya ufungaji taa, iendane na utengenezaji barabara,” amesema.
Amependekeza uwekaji taa ufanywe hata katika barabara za mitaa zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura).
Kuhusu miundombinu ya BRT awamu ya pili, amesema ujenzi wake umekamilika tangu Agosti na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inaendelea na mchakato wa kuleta mabasi.
Amesema tayari mtangulizi wake, Innocent Bashungwa ametoa ruhusa ya barabara hiyo kutumika na watumiaji wengine.
Msimamizi wa Miradi ya BRT kutoka
Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Frank Mbilinyi amesema kwa sasa mradi huo upo katika awamu ya tatu inayotarajiwa kukamilika Machi mwakani.
Amesema awamu ya nne kuelekea Tegeta inatekelezwa katika makundi matatu na tayari makandarasi wapo kwenye hatua mbalimbali.
“Kulikuwa na ucheleweshaji wa kujipanga kwa hiyo pengine hautakamilika Aprili mwakani, lakini wanaendelea vema, tunaamini utaenda sawa,” amesema.
Kuhusu mradi huo eneo la Ubungo na Kimara, amesema ilipangwa kukamilika Aprili mwakani na anaamini itakamilika ndani ya muda.
Kipande cha Msimbazi kwenda Chang’ombe, amesema kimeachwa kupisha ujenzi wa daraja kisha kitaendelea katika awamu ya tano.
Amesema mchakato wa kumpata mkandarasi wa awamu ya tano unaendelea kwa sasa.
Alipokagua mradi wa upanuzi wa Barabara ya Morogoro, Ulega ametoa siku tatu kwa mkandarasi kuhakikisha anaanza kufanya kazi usiku na mchana.
Amesema kwa sasa kuna kusuasua kwa kazi katika mradi huo kinyume cha masharti ya mkataba.
“Mkataba unasema hadi muda huu mkandarasi alipaswa kuwa amefikia asilimia 52 ya utekelezaji lakini yupo asilimia 26 hii haipo sawa.”
“Mkandarasi amezembea matakwa ya mkataba ni asilimia 52. Namuagiza aongeze kasi aweke taa kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana na nitakuja usiku kukagua nione kama anafanya hivyo,” amesema.
Amesema ikifanyika kinyume, atawachukulia hatua watendaji walio chini ya mamlaka yake.