Mwanza. Kitongoji cha Kishomberwa kilichopo katika Kijiji cha Kigazi, wilayani Missenyi, Kagera, Tanzania, kimekuwa na umuhimu mkubwa kutokana na Kituo cha Hija cha Mtakatifu John Marie Muzeeyi, Mtanzania wa kwanza kutangazwa mtakatifu na Kanisa Katoliki.
Kituo hiki huvutia maelfu ya waumini na watalii kila Januari, wakikumbuka maisha ya Muzeeyi na mashahidi wa Uganda waliouawa kwa imani yao.
Hija hii imeleta fursa kubwa kwa wakazi wa Minziro kupitia biashara, malazi, na huduma za utalii, huku hifadhi ya Misitu ya Asilia ya Minziro ikishirikiana na kanisa kutangaza vivutio vya asili, hivyo kuchochea uwekezaji na kuboresha maisha ya wanakijiji.
Hija ni miongoni mwa maneno maarufu kwa waumini wa dini mbalimbali ikimaanisha ibada inayofanyika sehemu maalumu kwa ajili ya maungamo, kutubu, kuomba dua, kusali au kuabudu.
Ibada hii inaweza kutekelezwa kwa kuzingatia tarehe maalumu kulingana na kalenda ya mwezi na mwaka kwa dini au madhehebu husika.
Kwa Waislamu, Kituo cha Hija ni Makka nchini Saudi Arabia ni maarufu ambapo waumini kutoka sehemu mbalimbali duniani humiminika kufanya ibada.
Wakristo wa madhehebu mbalimbali pia wanayo maeneo yao kadhaa ya hija ukiwemo mji wa Jerusalem nchini Israel, Mji wa Lourdes, Ufaransa au Namugongo, Kampala nchini Uganda walikouawa mashahidi 22 wa Uganda.
Hapa nchini, ukiacha eneo la hija la Nyakijoga mkoani Kagera, kipo Kitongoji cha Kishomberwa kilichoko katika Kijiji cha Kigazi, Kata ya Minziro wilayani Missenyi mkoani humo pia, ambacho ni eneo lingine la hija kwa waumini wa Kanisa Katoliki, ambalo linazidi kupata umaarufu likitembelea na maelfu ya watu kila mwaka.
Kwa mujibu wa Suleiman Rumanyika, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigazi Kata ya Minziro, umaarufu wa kijiji hicho kilichoko eneo la mpakani mwa Tanzania na Uganda, unafungamanishwa na historia ya mauaji wa mashahidi wa Uganda yaliyotokea Namugongo, Kampala kati ya Januari 31, 1885 na Januari 27, 1887.
Rumanyika anasema kwenye kitongoji hicho ndipo chimbuko na alipozaliwa Muzeeyi au Jean-Marie, mmoja wa waumini hao 22 wa Kikristo, waliouawa nchini Uganda wakati wa utawala wa Mfalme Kabaka Mwanga wa I, maarufu kama Mashahidi wa Uganda.
Miongoni mwa mashahidi hao wa Uganda waliokuwa wakitetea imani yao ya Ukristo, wapo waliouawa kwa kuchomwa moto, kukatwa kwa mapanga au kuchomwa mikuki kutokana msimamo wa kushika imani yao, iliyokuwa inakatazwa na utawala.
John Marie Muzeeyi anayetajwa kuwa mtu aliyekuwa na huruma na mkarimu kwa watu masikini na wenye ulemavu, aliuawa Januari 27, 1886 akiwa na umri wa miaka 36.
Rumanyika anaendelea kusema, kiongozi wa mashahidi hao waliouawa kwa nyakati tofauti, alikuwa Charles ‘Karol’ Lwanga na miongoni mwao alikuwemo John Baptisti Kizito, aliyeuawa akiwa na umri mdogo zaidi wa miaka 14, na hivyo kuweka historia ya kuwa shahidi aliyeuawa akiwa na umri mdogo kuliko wote.
Ibada ya Hija Kishomberwa
Enerika Kamajura (85), mzee anayeishi jirani na ilipo sehemu ya Hija katika kitongoji hicho, anasema kutokana na historia na kumbukumbu John Marie Muzeeyi, Kanisa Katoliki limejenga mnara wa sanamu yenye sura ya shahidi huyo katika eneo alikozaliwa, ambako waumini kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi hufika kwa ajili ya hija kila Jumapili ya mwisho ya Januari kila mwaka.
Anasema, uwepo wa mnara wa kumbukumbu na Kituo cha Hija cha John Marie Muzeeyi, ni sifa si tu kwa Kitongoji cha Kishomberwa, bali pia kwa Taifa kwa sababu shahidi huyo ndiye Mtanzania pekee aliyetangazwa kuwa mtakatifu kwa mujibu wa Imani ya kanisa hilo. Alitangazwa utakatifu na Papa Paul VI Oktoba 18, 1964.
“Kwa waumini wa Kanisa Katoliki, Kitongoji cha Kishomberwa kina hadhi na historia hao mashahidi 22, akiwemo Muzeeyi,” anasema na kuongeza: “Umuhimu huo ndiyo huwafanya maelfu ya watu wafike hapa kila mwaka kufanya Hija.”
Kituo cha Hija katika Kitongoji cha Kishomberwa si tu ni muhimu kiimani, bali pia ni fursa ya utalii wa kiimani kutokana eneo hilo kutembelewa na waumini kutoka ndani na nje ya nchi, kama anavyoeleza Hassan Omary, mhifadhi wa mazingira asilia Minziro kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Hifadhi ya Misitu Asilia ya Minziro inayopakana na vijiji vinane pia hunufaika na uwepo wa Kituo cha Hija cha John Marie Muzeeyi kwa sababu wageni na waumini wanaokwenda na kutoka Kishomberwa, lazima wapite katikati ya hifadhi hiyo inayomilikiwa na kusimamiwa na TFS.
Kutokana na uhusiano asilia uliopo kati ya Kituo cha Hija cha John Marie Muzeeyi na Hifadhi ya Misitu Asilia ya Minziro, uongozi wa Kanisa Katoliki kupitia Parokia ya Minziro unashiriki katika kutangaza vivutio vya utalii na fursa zinazopatikana eneo hilo.
Pamoja na maelezo kwa njia ya mdomo, uongozi wa TFS pia hugawa vipeperushi na majarida yenye maelezo na taarifa za shughuli za uhifadhi kwa waumini kutoka sehemu ndani na nje ya nchi wakati wa ibada ya Hija.
Kutokana na hija inayofanyika kila Januari kuwa kubwa inayokusanya wageni zaidi ya 10,000, kijiji kinapata manufaa makubwa.
“Kwa ujumla tunapata faida sana, kwanza kwa mwananchi wa kawaida wa Minziro inapofika siku hiyo tunauza biashara zetu, wageni wanalala pale, tunasheherekea, tunafurahi, tunakula na kunywa.
“Sisi wana Minziro tunafaidi kwa kweli hata Serikali inatambua huyu siyo shahidi wa Minziro tu ni shahidi wa Tanzania. Hata Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameshawahi kutuunga mkono kwa kutuletea umeme,” anasema Rumanyika.
Hata hivyo, anasema bado wanaomba kupatiwa huduma ya maji na eneo hilo liboreshwe kwa kujengwa kumbukumbu ya kanisa kubwa zaidi, baada ya wanakijiji wamechangia kuchangia nguzo nane ambazo hazijasimama.