Wanne mbaroni wakidaiwa kuhujumu miundombinu ya Tanesco, SGR

Dar es Salaam. Watu wanne wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa vipindi tofauti wakidaiwa kuhujumu miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mara kadhaa TRC imekuwa ikieleza kuwapo kwa baadhi ya watu wanaokula njama za kuharibu miundombinu ili kuzorotesha usafiri wa treni ya kisasa (SGR).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkoa wa Kipolisi Rufiji, watuhumiwa wawili walikamatwa Desemba 13, 2024 wakiwa na vipande vya shaba 426 vyenye uzito wa kilo 7,728 na nyaya za shaba zenye uzito wa kilo 2,628.5 zilizotambuliwa kuwa ni mali zilizoibwa kutoka kwenye miundombinu ya Tanesco.

Pia wanadaiwa kukamatwa na nyaya za shaba za TRC zenye uzito wa kilo 430 na vipande vya shaba vilivyotengenezwa kutoka kwenye nyaya ambazo zimeibiwa Tanesco na TRC ili kuficha uhalisia wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa jana Desemba 14, 2024 watuhumiwa walipataikana baada ya kukamatwa gari aina ya Fuso lililobeba shehena ya vipande na nyaya za shaba walizotoa kiwandani kwao.

“Gari hilo lilikuwa linatoka kiwandani kwao kwenda kuzificha baada ya kuona operesheni kali ya Polisi inayoendelea,” imesema taarifa hiyo.

Wawili hao wanadaiwa kukamatwa ikiwa ni saa chache tangu jeshi hilo kutangaza kuwashikilia watuhumiwa wengine wawili wenye asili ya Asia Desemba 12, 2024 katika Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Kipolisi Rufiji.

Katika tukio la awali raia hao wa kigeni wanadaiwa kukutwa na nyaya za shaba ambazo zilitambuliwa kuhujumiwa kutoka miundombinu ya Tanesco na TRC zilizokutwa katika kiwanda chao.

Wawili hao walikutwa na nyaya za shaba za Tanesco zilizokuwa na kilo 608.6 na kilo 5,500.17 za TRC.

Hatua hiyo inaelezwa ni mwendelezo wa operesheni zinazofanywa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kulinda miundombinu hiyo, ili kuhakikisha usafiri wa treni ya umeme unafanya kazi katika ufanisi unaotakiwa.

Treni ya SGR ambayo inafanya safiri kati ya Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma ilikuwa na changamoto iliyoathiri ratiba za wasafiri.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa akizungumza na Mwananchi Novemba 5, alisema kuna njama zinazofanywa kwa lengo la kuhujumu mradi huo.

Kadogosa alisema hujuma hizo si za hivi karibuni, bali zilianza muda mrefu huku akieleza baadhi ya wahusika wamekamatwa ambao wako mbioni kuchukuliwa hatua.

Kadogosa alisema kumekuwa na sintofahamu ikiendelea, wengine wakihisi kuna mgawo wa umeme kwenye SGR.

“Kuna nyaya zilikatwa kwenye eneo kati ya Soga na Pugu na waliofanya hivyo si vibaka, ni watu wenye nia ya kuhujumu mradi huu na wanajua walichokuwa wanakifanya.

“Kuna ambao tumeshawakamata na ushahidi upo, na hii si mara ya kwanza, hatukutaka kuwatangaza kwa sababu tulihitaji ‘tu-dili’ nao kimyakimya, hatua dhidi yao zinaendelea na watakapohukumiwa wananchi watawafahamu,” alisema akieleza hujuma ndizo zimekuwa zikiathiri safari za treni hiyo.

Katika kukabiliana na hilo, Novemba 9, 2024 wabunge waliiagiza TRC kufunga kamera za ulinzi mara moja maeneo yote ya reli ili kukabiliana na watu wanaohujumu miundombinu ya SGR.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Miundombinu, Selemani Kakoso alisema kufungwa kwa kamera za ulinzi (CCTV) kutawezesha kukabiliana na hujuma kwa mradi huo.

Kakoso alisema mbali ya kamera, uwekwe ulinzi wa mfumo wa umeme ambao wote wanaotaka kuihujumu reli hiyo wanaswe na mifumo ya umeme.

“Hii itasaidia sana kwa sababu sisi

Watanzania kuna watu ambao bado hawaoni umuhimu wa kutunza hii miundombinu, ndiyo maana watu wanashuhudia mradi mkubwa unaweza kujengwa kwenye barabara, eneo lote ambalo wameweka vibao ambavyo vinawasaidia hata wenyewe, wanakuja kutoa na kwenda kuuza kama chuma chakavu.

“Vitu hivi havitusaidii kwa sababu Serikali imewekeza fedha nyingi ikiwemo kuahirisha kufanya mambo mengine ili kuimarisha mradi huu. Hivyo, watu wanapaswa kuelewa kiwa mradi tulionao ni wa kwetu sote si wa TRC pekee,” alisema.

Safari ya kwanza ya treni ya umeme ilianza Juni 14, 2024 kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ikiwa na mabehewa 14 yaliyojaa. Julai 25, 2024 treni hiyo ilianza safari za Dar es Salaam hadi Dodoma.

Related Posts