Wanne tu wanatosha Transit Camp

KAIMU Kocha Mkuu wa Transit Camp, Emmanuel Mwijarubi amesema katika dirisha hili dogo la usajili timu hiyo inahitaji kuongeza nyota wanne katika nafasi mbalimbali, zitakazowasaidia kuwatoa chini mwa msimamo na kusogea angalau juu zaidi.

Kocha huyo anayekiongoza kikosi hicho baada ya Ally Ally kutimuliwa kutokana na mwenendo mbaya, alisema maeneo ambayo anahitaji yaboreshwe ni beki wa kulia, viungo wawili kwa maana ya mkabaji na ushambuliaji na mshambuliaji pekee wa kati.

“Hatuko katika sehemu nzuri kutokana na matokeo ambayo tunayapata ingawa ukiangalia kwa sasa kuna matumaini makubwa kwa sababu aina pia ya uchezaji imebadilika, nimekabidhi ripoti hiyo nikiamini ni maeneo tunayopaswa kuyazingatia,” alisema.

Mwijarubi aliyekiongoza kikosi hicho katika mchezo wake wa kwanza juzi na kulazimishwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Mbuni ya Arusha, alisema baada ya kukaa na wachezaji wamemuahidi kupambana na kuhakikisha timu hiyo inasogea nafasi za juu.

Timu hiyo iliyocheza michezo 12 hadi sasa, imeshinda mchezo mmoja tu, sare minne na kupoteza saba ikifunga mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 16, ikishika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi ya Championship na pointi saba.

Related Posts