Waomba mazingira rafiki uchaguzi mkuu 2025, tume yafafanua

Mbeya. Wakati watu wenye uhitaji maalumu wakiomba kuwekewa mazingira rafiki kushiriki mchakato wa kupiga kura, viongozi wa dini nao wameomba kupewa utaratibu wa kushiriki rasmi siasa wakidai ni sehemu ya maisha.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 15, 2024 wakati wa mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura uliofanyika mkoani Mbeya.

Akizungumza kwa niaba ya viziwi, Atusajigwe Mwalegwa amesema katika mchakato wa uchaguzi wanakosa mawasiliano kwenye maeneo ya kutoa huduma ambako hakuna wasaidizi kwa wenye uhitaji.

“Sisi viziwi tunakosa haki zetu katika uchaguzi sehemu ya vituo hakuna wasaidizi, nashauri uchaguzi mkuu ujao wawepo wakalimani kwa msaada zaidi tupate haki yetu kikatiba,” amesema Atusajigwe.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha wasioona Mkoa wa Mbeya (TLB), Yohana Mwonga amesema bado miundombinu ya watu wenye ulemavu ngazi za chini si rafiki licha ya mwongozo unaotolewa.

“Mwongozo unatolewa juu, lakini huku chini utekelezaji hakuna, tunaomba tunapoelekea uchaguzi mkuu ujao kuwepo vifaa saidizi haswa kwetu wasioona,” amesema Mwonga.

Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Ualbino mkoani humo, Claudi Mwakyoma amesema wakati wa hatua ya upigaji kura kada hiyo hupanga foleni tena katika mazingira magumu.

“Jua kwetu linatuathiri sana, hatuna ile nafasi ya kupewa kipaumbele, tunaomba mwakani kada hii ipewe nafasi tusiwekwe foleni kwenye jua kwani ni hatari kwetu,” amesema Mwakyoma.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) Mkoa wa Mbeya, Sheikh Ibrahim Bombo amesema licha ya tume kuitambua kada ya viongozi wa dini kama mdau, lakini inawataka kutohusisha siasa na dini.

“Turuhusiwe kujihusisha na siasa kwa kuwa nayo ni sehemu ya maisha kwa utaratibu, tunaona bungeni wapo viongozi wa dini,” amesema Sheikh Bombo.

Akijibu kero na hoja hizo, Mkurugenzi wa Tume huru ya Uchaguzi, Kailima Ramadhan amesema licha ya changamoto za walemavu, lakini Tume hiyo inaenda kuyafanyia kazi kutokana na uboreshaji daftari la kudumu la wapigakura.

Kuhusu viongozi wa dini, Ramadhan amesema kada hiyo haizuiwi kujihusisha na siasa bali kuhubiri na kutangaza siasa sehemu za ibada.

“Ni kweli changamoto zipo, ila imeelekezwa kwa yeyote mwenye tatizo awe na msaidizi wake kumuelekeza ili atimize haki yake ya kikatiba kuanzia kujiandikisha hadi kupiga kura”

“Viongozi wa dini haijakatazwa kujihusisha na siasa, bali ile kuhubiri madhabahuni au kwenye mimbari kuhamasisha siasa ndio haitakiwi,” amesema Ramadhan.

Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele amevitaka vyama vya siasa kuhamasisha wananchi kushiriki maboresho ya daftari la kudumu la wapigakura.

Mwambegele amesema kuwa hadi sasa mikoa 21 imeshafikiwa katika akieleza kuwa matarajio yao ni kuona makundi maalumu yanapewa kipaumbele.

“Kuweni mabalozi kwa wananchi katika kuhamasisha kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura, watoa huduma watatoa kipaumbele kwa makundi maalumu.

“Lazima ieleweke, kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa la jinai na adhabu yake ni kulipa Sh100,000 hadi Sh300,000 au jela miezi sita au vyote kwa pamoja,” amesema.

Related Posts