Waziri aruhusu kupigwa muziki nyakati za sikukuu Zanzibar

Waziri wa Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita ametoa ruhusa ya upigaji wa muziki katika siku nne za Sikukuu ya Krismas sambamba na siku mbili za kusherehekea mwaka mpya huku ikizingatia uthibiti wa sauti ili isiwe kero kwa Jamii.

kauli hiyo ameitoa katika ukumbi wa kituo cha Elimu Amali Makunduchi wakati wa kikao cha majadiliano ya kukusanya maoni ya wadau mbali mbali ikiwemo wamiliki wa Mahoteli, Nyumba za Starehe (Mabaa) pamoja na wapigaji wa mziki.

Amesema kuwa ruhusa hiyo ameitoa kwa kipindi kifupi cha sikukuu ikimalizika wataendelea na zuwio hilo hadi utapotolewa uwamuzi na utaratibu maalum kwa mujibu wa maagizo ya Serikali .

Aidha amewataka wamiliki hao kufuata utaratibu wa uthibiti wa sauti kwa mujibu wa muongozo wa uthibiti wa sauti (volume 40) walipewa ili wasiathiri uhuru wa wageni na wananchi wengine.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni (BASSFU) Juma Chum Juma amesema atahakikisha anasimamia miongozo iliyowekwa ili wamiliki waweze kufuata utaratibu ambao unakwenda sambamba na kanuni na sheria za baraza hilo

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Othmani Ali Maulid ameahidi kusimamia muongozo uliotolewa na serikali ili wilaya hiyo ibaki kuwa salama.

Amesema iko haja ya wamiliki hao kufuata masharti waliopewa na serikali juu ya namna bora ya upigaji wa muziki ili kutowakera wageni ambao wanahitaji mapumziko katika hoteli zao.

Akitoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya kusini kutoa mashirikiano ya pamoja iwapo watabaini kuna kitu ambacho kinaashiria uvunjifu wa Amani kutoa taarifa katika mamlaka husika .

Nao wamiliki hao wamesema wataendelea kushirikiana na serikali kwa kufuata muongozo na taratibu zilizopo na kumuomba waziri awaruhusu katika kipindi hichi cha msimu wa sikukuu ili waweze kuingiza pesa za kulipia kodi zao .

Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni (BASSFU) ilitoa taarifa ya kuzuwia muziki katika mahoteli ya kulaza wageni, nyumba za starehe pamoja na wapigaji wa miziki mnamo Oktoba 18,2024. kwa wamiliki wote wa Zanzibar.

Related Posts