Yakifanyika haya uchumi wa soko utazalisha ajira kwa Watanzania

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud ametaja mambo kadhaa ambayo yakifanyika Taifa litafanya vizuri katika uchumi utakaozalisha ajira kwa Watanzania.

Mambo hayo ni sera,  mfumo, sheria , uongozi bora katika kutunga na kusimamia sera, utendaji wenye ufanisi, teknolojia sahihi kwenye uzalishaji na udhibiti na uimara wa mfumo mzuri wa kikodi.

Othman ameeleza hayo leo Jumapili Desemba 15, 2024 alipofungua mkutano wa nne wa kumuenzi Maalim Seif Sharif Hamad uliofanyika mjini Unguja ukiwa na mada ya ‘Demokrasia, uchumi wa soko huru, ajira, changamoto na fursa’.

Hii ni mara ya nne maadhimisho hayo yanafanyika tangu kufariki dunia Maalim Seif aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa ACT- Wazalendo ambacho ni chama kikuu cha upinzani Zanzibar.

Maadhimisho hayo yameandaliwa na Taasisi ya Maalim Seif Foundation ikishirikiana na Taasisi ya Friedrich Naumann. Yamekuwa yakifanyika kila mwaka tangu Februari 17, 2021.

“Kitu kimoja kinachoshindaniwa katika soko huria ni namna ya kuwa na sera bora zitakazowavutia wenye mitaji, wazalishaji na soko lenu na uwezo wa kulihudumia.”

“Pia lazima kuwa na uongozi wenye maono utakaotunga sera na sheria sahihi, kuweka miundombinu ya usimamizi ya sera zenyewe,” amesema Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo amesema bila kuwepo utendaji wenye ufanisi siyo rahisi kuyafikia hayo.

“Tumeona katika nchi kunaweza kukawa na kila kitu, ikiwemo ardhi ya kutosha ya uzalishaji, suala linakuwa kwenye teknolojia ya kuzalisha. Inawezekana tunaweza kuwa na rasilimali za uzalishaji, suala linakuja tunawezaje kutumia katika kuzalisha?” amesema.

kwa dunia ya sasa, amesema lazima kuwepo ubora unaostahili ili kulitumia soko hilo la ushindani.

“Katika kila kitu suala la ubora kwa kile tunachokizalisha na matumizi ya teknolojia ni muhimu,” amesema.

Amesema kwa dunia ya sasa ili kuvutia uwekezaji hata kwa kutumia rasilimali zako, ili kuwashawishi wenye fedha kuweka mitaji ni muhimu kuwa na mfumo mzuri wa kikodi utakaohakikisha mtu anapowekeza fedha zinakuwa salama.

“Lazima kuwe na uimara katika mfumo wetu wa kikodi uwe unafahamika, siyo leo asilimia tano kesho 15 au 20 hadi 30. Uimara katika kodi ni muhimu sana kama tunataka kutengeneza uchumi wa soko huria,” amesema.

Kuhusu demokrasia amesema lazima taasisi husika zifikie moja ya misingi ya demokrasia itakayojenga na kuzalisha uchumi wa soko huria kwa kuhakikisha kunakuwa na utawala wa sheria, uwajibikaji katika ngazi zote na uwazi.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mohamed Aboud amesema Maalim Seif alikuwa kiongozi aliyetaka kuona haki, uadilifu na maendeleo kwa Taifa na wananchi wake.

Amesema suala la demokrasia, uchumi na ajira ni muhimu katika Taifa hususan Zanzibar.

“Mada hizi zitafanikiwa ikiwa tutaimarisha umoja wetu, jambo la msingi zaidi ni kuimarisha umoja,” amesema.

Amesema kwa Zanzibar mara nyingi umoja umekuwa ukitetereka na huwa unapotea wakati unapofika uchaguzi, kwa hiyo jitihada zinapaswa kuongezwa hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Halifanyiki jambo lolote bila amani, kwa hiyo tunapozungumza mada hizi tuweke mkazo wa kuzungumzia umoja huu ili ukue badala ya kutetereka.”

“Nayasema haya kwa sababu zimeanza kuonekana dalili kwa hiyo ni wakati wa vyama vya siasa kukaa pamoja kuzungumza ili kudumisha umoja ambao utachangia maendeleo yetu,” amesema.

Amesema siasa siyo ugomvi bali ni kukidhi matarajio na mahitaji ya wananchi, iwapo yakifanyika ambayo hayana faida kwao haiwezi kuwa siasa, hivyo amehimiza vyama vya siasa kukaa pamoja kuzungumza mambo ambayo wanaona yana shida.

“Tusichoke kuzungumza, kwenye mazungumzo ndiyo tunapata kujadili mambo yetu na kupata mwelekeo mmoja,” amesema.

Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Maalim Seif, Nassor Ahmed Mazrui amesema dunia nzima inataharuki kuona demokrasia inapitia changamoto ikizingatiwa ina nafasi kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kukuza ajira.

Amesema demokrasia imeathiri ukuaji wa uchumi, hivyo kuwa na demokrasia ya kweli lazima itengeneze mazuri katika nchi.

“Tuyajadili haya, tuseme ukweli na kuwa na demokrasia ya kweli, Maalim alikuwa muumini wa demokrasia aliiamini inakuza uchumi, ametuachia urithi mwema kwa hiyo tuendelee kumuenzi,” amesema.

Mkurugenzi Mkazi wa National Democratic Institute (NDI), Sandy Quimbaya amesema katika kukuza demokrasia ipo haja ya kushirikiana na kushughulikia changamoto zinazojitokeza kila wakati.

Mkuu wa Ofisi ya Friedrich Nauman Foundation for Freedom, Stefan Schott amesema demokrasia siyo kazi rahisi lakini ni muhimu kuzingatia utawala wa sheria.

Amesema kwa nchi za Afrika bado kuna changamoto ya demokrasia hivyo ipo haja kuhamasishana katika kuikuza.

Related Posts