Yanga ina dakika 270 tu CAFCL

YANGA imesaliwa na dakika 270 za kufa au kupona kama inataka kwenda robo fainali kutoka Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya jana kuambulia pointi moja dakika za jioni baada ya mtokea benchi, Prince Dube kuchomoa bao na kuinyang’anya tonge mdomoni, TP Mazembe ya DR Congo, jijini Lubumbashi.

Dube aliyekuwa hajafunga katika mechi 13 mfululizo zilizopita zikiwamo 11 za Ligi Kuu na nyingine mbili za CAF hatua hiyo ya makundi, lakini jana aliipata ‘code number’ kwa kufunga bao hilo dakika za majeruhi na kuiokoa timu hiyo iliyopasuka mechi mbili mfululizo ya Kundi A, kwani ingekuwa aibu kwa klabu hiyo.

Yanga imecheza makundi ya Ligi ya Mabingwa katika msimu ya mwaka 1998, 2023-2024 na msimu huu, lakini ilishacheza pia mara tatu Kombe la Shirikisho 2016, 2018 na 2022-2023 ilipofika fainali na kulikosa taji mbele ya USM Alger kwa kanuni ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni 2-2, Yanga ikishinda ugenini 1-0 na kufungwa nyumbani 2-1.

Katika mara zote ilipocheza makundi ilikuwa haijawahi kupoteza mechi mfululizo, kabla ya Dube kufanya yake na kuiokoa dakika ya jioni.

Kabla ya sare ya jana, Yanga ilishapoteza mechi mbili za kundi hilo ikifungwa 2-0 nyumbani na ugenini na Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria mtawalia na sasa imesaliwa na michezo mitatu ya kuamua hatma yake katika kundi hilo linaloongozwa na Wasudan waliokuwa uwanjani usiku wa jana kuikaribisha Mc Alger.

Lile soka tamu la kushambulia kwa kasi na kukaba kuanzia juu, ni kama limepotea kwa Vijana wa Jangwani tangu kocha Sead Ramovic kuchukua mikoba ya Miguel Gamondi aliyefurushwa hivi karibuni baada ya Yanga kupoteza mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam (1-0) na Tabora United waliowafunga 3-1.

Katika mchezo wa jana Yanga ilikuwa inapoteza mipira mingi mbele ya wachezaji wa timu wenyeji, huku kipa Diarra Djigui akitumika kwa dakika 45 tu baada ya kuumia akiwa tayari ameshatunguliwa bao hilo lililofungwa dakika ya 41 na mtokea benchi Cheikh Fofana aliyeingizwa dakika ya 39 baada ya Gloire Mujaya kuumia.

Kocha Ramovic alimtoa Diarra pamoja na Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya na kuwaingiza Abubakar Khomeiny, Clement Mzize na Stephane Aziz KI kabla ya kuwatoa tena Kennedy Musonda na Duke Abuya na kuwaingiza Prince Dube na Clatous Chama ambao waliongeza kasi ya mashambulizi lakini hayakuisaidia kitu.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mazembe, kiungo Khalid Aucho aliyekosa michezo miwili iliyopita alianza kikosi cha kwanza sambamba na Dickson Job ambao hawakutumika mechi iliyopita dhidi ya Mc Alger, huku Aziz KI akianzia benchi, huku timu ikiwa haionyeshi makali yaliyozoeleka enzi za Gamondi.

Sare hiyo ya jana licha ya kuifanya Yanga kuendelea kusalia mkiani mwa kundi hilo ikiwa na pointi moja, huku Mazembe ikifikisha mbili kila mmoja ikicheza mechi tatu, lakini haikufurahisha mashabiki wa klabu hiyo kutokana na soka inalocheza kwa sasa timu chini ya Ramovic.

Yanga itarudiana na Mazembe wiki ijayo kabla ya kumalizana na MC Alger na kisha Al Hilal ambazo ni lazima zishinde kama inataka kutinga robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo baada ya awali kufanya huivyo msimu uliopita chini ya kocha Gamondi aliyeifikisha makundi ya msimu huu kabla ya kutimuliwa.

Katika kipindi cha kwanza kwa mechi ya jana Mazembe ilitawala sehemu kubwa ya mchezo, huku Yanga ikitengeneza nafasi chache, huku kipa Diarra akionekana kama ameumia na kuomba kutolewa kabla ya kuachwa amalize dakika 45 na kutolewa sambamba na wenzake wawili.

Kipindi cha pili baada ya mabadiliko hayo angalau Yanga ilionyesha uhai kwa kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini zikawa zinapotezwa kutokana na umakini mdogo waliokuwa nao, Pacome Zouzoua na Mzize kabla ya Dube kusahihisha makosa wakati Mazembe wakisubiri filimbi ya mwisho kusherehekea ushindi wa kwanza, kwani walishapoteza mechi moja iliyopita dhidi ya Al Hilal na kuambulia sare mbele ya MC Alger.

Vikosi vilivyocheza jana;

MAZEMBE: Badara Faty, Johnson Atibu, Merceil Ngimbi/Abdallah Fabrice, Boubacar Hainikoye, Oscar Kabwit, Boaz Ngalamulume, Oussein Badamassi/Zemanga Soze, Gloire Mujaya/Cheikh Fofana, Ernest Luzolo, Magloire Ntwambe(c)na Sosue Mungwengi

YANGA: Diarra Djigui/Abukabar Khomeiny, Yao Kouassi, Nickson Kibabage, Ibrahim Job, Dickson Job (c), Khalid Aucho, Maxi Nzengeli/Clement Mzize, Duke Abuya/Clatous Chama, Kennedy Musonda/Prince Dube, Mudathir Yahya/Stehpane Aziz KI na Pacome Zouzoua

Related Posts