Ahadi ya Serikali kurahisisha utaratibu biashara changa

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko ametoa maagizo matatu kwa wizara yanayolenga kutatua changamoto zinazolalamikiwa na wabunifu wa biashara changa na bunifu (startup), ikiwemo kukosekana mitaji.

Maagizo hayo yanalenga kutengeneza mazingira rafiki na kurahisisha ufanyaji wa biashara kusaidia ukuaji wa uchumi na kuzalisha ajira kwa vijana.

Maagizo hayo ni kuandaa mifumo ya kisera na kisheria ili kuhamasisha ukuaji wa ikolojia ya startup nchini, Wizara ya Fedha kuangalia namna ya upatikanaji wa mikopo na ujumuishaji wa kundi hilo, katika manunuzi ya asilimia mbili yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza leo Desemba 16, 2024 wakati wa uzinduzi wa wiki ya Startup Tanzania, Dk Biteko amesema pamoja na mafanikio yanayoonekana, bado zipo hatua zinazowakwaza wabunifu ikiwemo sheria ambazo wakati mwingine zinatengeneza urasimu usiokuwa na maana.

Kutokana na hilo, aliitaka Wizara ya Mipango na Uwekezaji kwa kushirikiana na wadau wengine ndani na nje ya Serikali kuanza mchakato wa kuandaa mifumo ya kisera na kisheria ili kuhamasisha ukuaji wa ikolojia ya startup nchini.

“Mifumo hii itoe tafsiri sahihi ya startup, uwezeshwaji unaohitajika pamoja na kubuni vivutio maalumu kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika sekta hii,” amesema.

Dk Biteko ameitaka Wizara ya Fedha kuangalia njia za kutatua changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa startup na kufanya maboresho ya mifumo ya kodi, ili kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka kwa wawekezaji wa mitaji ya ubia na kampuni za hisa binafsi.

Hilo linafanyika wakati ambao Serikali kwa kutambua umuhimu wa mfumo thabiti wa kifedha na mitaji, imetekeleza sera na mifumo mbalimbali ya kimkakati ambayo inawezesha suala hilo.

Miongoni mwa yaliyofanyika ni Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (2020/21-2029/30) ambao umeboresha uthabiti, ufanisi na ushirikishwaji wa sekta ya fedha kuhakikisha kuwa startup zinapata mitaji inayohitaji ili kuwezesha kukua.

“Vilevile mkakati wa ufadhili wa biashara Ndogo za Kati (SME) umeundwa ili kuziba pengo la ufadhili kwa biashara hizi na kuwapatia rasilimali za kupanua shughuli zao na kuchangia kikamilifu katika uchumi,” amesema Dk Biteko.

Amesema mikakati hiyo imeimarishwa na Mfumo wa Kitaifa wa Ushirikishwaji Kifedha (NFIF I,II,III) ambao NFIF III (2023-2028) inayotumia huduma za kifedha za kidijitali kuwaleta Watanzania wengi zaidi kwenye uchumi rasmi.

Katika maagizo yake ya mwisho alitaka kupitiwa upya kwa kanuni za ununuzi wa umma 2016 ili kuhakikisha startup zinajumuishwa kikamilifu katika makundi maalumu, yakiwemo ya vijana na biashara zinazoongozwa na wanawake.

Haya yote yanafanyika ili kuziwezesha biashara hizo changa kujiendeleza, akiwaita vijana kuangalia changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii na kuzitafutia suluhisho.

Jambo hilo litasaidia kuzalisha ajira nyingi kwa vijana, akieleza kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kupunguza pengo la ajira kwa vijana.

Mkurugenzi wa Tanzania Startup Association (TSA), Zahoro Muhaji amesema wanaishukuru Serikali kwa kuonyesha utayari na kuamua kuanzisha mfuko rasmi wa mitaji kwa ajili yao.

“Mfuko huu utasaidia upatikanaji wa fedha za uwekezaji kutoka kwa Serikali jambo ambalo linapaswa kupongezwa,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya TSA, Paul Makanza amesema ni wakati wa kuwekeza kwenye startups ili baadaye wavune+ faida zake.

“Wadau wa kimataifa ombi letu ni kuwa tuzidi kushirikiana na wale wa taasisi za elimu, moja ya kitu tunachoweza kufanya ni kuwa na ushirikiano kwani vyuo ndiyo chimbuko la mawazo mengi ya kibunifu,” amesema.

Related Posts