YANGA imerejea asubuhi ya jana ikitokea Lubumbashi, DR Congo ilikopata pointi moja ya kwanza karika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kocha wa timu hiyo na nahodha msaidizi wakitoa msimamo juu ya nafasi ya kutinga robo fainali kwa mara ya pili mfululizo.
Yanga iliyopoteza mechi mbili za awali za Kundi A mbele ya Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria, kila moja ikiichapa mabao 2-0, juzi ilizinduka kwa TP Mazembe kwa kuinyang’anya tonge mdomoni ikichomoa bao katika dakika ya mwisho ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mazembe, likifungwa na Prince Dube.
Mara ya mchezo huo kikosi hicho kilianza maandalizi ya kurudi nyumbani na kikatua jana saa 5 asubuhi, ambapo beki wa kati na nahodha msaidizi, Dickson Job na kocha Sead Ramovic, kila mmoja akitoa msimamo walipozungumza na Mwanaspoti kwenye Uwanja wa Ndege mara walipowasili.
Job alisema pointi moja waliyoipata kwa Mazembe itawarudishia hali ya kujiamini na wanaanza mapema kupiga hesabu ya kuzisaka pointi tisa katika mechi tatu za mwisho ili kutimiza lengo la kwenda robo fainali.
Job alisema baada ya kupoteza mechi mbili za awali za kundi hilo, ziliwakata stimu na kurudisha chini morali, lakini kwa sare waliyopata ugenini juzi, kama wachezaji wanaona bado kuna nafasi ya kuzipigania mechi tatu zilizosalia, zikiwamo mbili za nyumbani na moja ya ugenini dhidi ya vinara wa kundi hilo, Al Hilal.
“Hakuna kitu kilichokuwa sawa kwetu baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo, kwani tulipungua nguvu, huu ndio ukweli lakini tunawashukuru makocha na viongozi walitujenga kisaikolojia wakati wote,” alisema Job na kuongeza;
“Inawezekana ikawa pointi moja, lakini ina maana kubwa sana kwetu, kwani ni bora kuipata kuliko kupoteza zote, tunarudi kujipanga kwa mechi zijazo tukianzia na hizi za ligi ambazo zitatupa nguvu ya kurudi na gia kubwa kimataifa.”
Ratiba inaonyesha Yanga itakuwa na mechi tano mfululizo, zikiwa nne za Ligi Kuu na moja ya Kombe la Shirikisho kabla ya kurudiana na Mazembe mapema Januari mwakani.
Mechi nne za Ligi itakazocheza Yanga ni ile wa Alhamisi dhidi ya Mashujaa, kisha Desemba 22 itaumana na Tanzania Prisons kabla ya kusafiri hadi Dodoma kupambana na Dodoma Jiji siku ya Krismasi halafu itarudi nyumbani kuipokea Kagera Sugar Desemba 29, hapo ni mbali na mechi ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho.
Yanga imepangwa kucheza na Copco ya Mwanza kabla ya mwaka 2024 kumalizika, kama ilivyo kwa watani wao Simba ambao wamepangwa kuvaana na Kilimanjaro Wonderers, japo tarehe hazifahamika hadi sasa.
Kocha Ramovic alisema mchezo wa juzi dhidi ya Mazembe kama wachezaji wa kikosi hicho wangekuwa utulivu, basi walistahili ushindi baada ya kuumiliki mchezo kwa muda mrefu wakishindwa kutumia nafasi walizozitengeneza langoni mwa wenyeji wao hao, walioenda mapumziko wakiongoza bao 1-0.
“Kuna kitu kinaendelea kujengeka taratibu ndani ya timu, lakini ukweli ni kwamba tulistahili ushindi.kama tungetumia nafasi tulizozitengeneza,” alisema Ramovic.