Dar es Salaam. Washtakiwa wanane katika kesi ya wizi wa mafuta katika visima kampuni ya kimataifa ya kuhifadhi mafuta, Tiper Tanzania Ltd (Tiper), wataendelea kusubiri hatima ya upelelezi wa kesi yao mpaka Desemba 30, 2024.
Washitakiwa hao, aliyekuwa dereva wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Tino Ndekela, mfanyabiashara Fikiri Kidevu, Amani Yamba, Mselem Abdallah, Kika Sanguti, Twaha Salum, Gaudence Shayo na Hamisi Hamisi, wanakabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu.
Katika kesi hiyo, wanakabiliwa na mashitaka 20 yakiwemo ya kutakatisha fedha na wizi wa mafuta ya petroli na dizeli zaidi ya lita milioni 9.9 na kuisababishia hasara kampuni ya Tiper ya zaidi ya Sh26 bilioni.
Kesi hiyo imetajwa leo Jumatatu, Desemba 16, 2024 kwa ajili ya kuangalia iwapo upelelezi umeshakamilika, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Frank Romuli ameieleza mahakama kuwa bado haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mkazi Mkuu, Ana Magutu kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, anayesikiliza shauri hiyo ambaye leo hakuwepo, ameahirisha kesi mpaka Desemba 30, 2024 itakapotajwa kuangalia hatima ya upelelezi na washtakiwa wataendelea kubaki mahabusu.
Washtakiwa hao wanaowakilishwa na wakili wa kujitegemea, Hassan Kiangio walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Oktoba 22, 2024 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Katika mashtaka hayo, mashtaka mawili ni ya uharibifu wa mali wanayodaiwa kutenda kati ya Januari mosi, 2019 na Desemba 31, 2022 eneo la Tungi- Kigamboni, wakidaiwa kuharibu bomba la kusafirishia mafuta aina ya petroli na dizeli, mali ya kampuni ya Tiper.
Pia wanakabiliwa na mashitaka 16 ya wizi wa mafuta wakidaiwa kuiba lita 3,599,458 za mafuta ya petroli na lita 6,392,356 za dizeli yaliyokuwa yakishushwa kutoka katika meli yakipitishwa katika visima vya kampuni hiyo ya Tiper.
Vile vile, wanakabiliwa na shtaka la kuisababishia kampuni hiyo ya Tiper hasara ya zaidi ya Sh26.01 bilioni, wakidaiwa kutenda kosa hilo tarehe hizohizo eneo la Tungi- Kigamboni, Dar es Salaam.
Pia wanakabiliwa na shtaka moja la kutakatisha zaidi ya Sh20.73 bilioni, kosa wanalodaiwa kulitenda katika tarehe hizo na eneo hilo, huku wakijua fedha hizo zilitokana na kosa tangulizi la wizi.
Tiper ni kampuni ya kimataifa ya kuhifadhi mafuta aina ya dizeli na petroli, inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzia kupitia Msajili wa Hazina na kampuni ya Oryx Energies SA ya Geneva, Uswis.