Waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar amesema uamuzi huo umechukuliwa kutokana na sera zisizo rafiki za Ireland. Mwezi Mei, Israel ilimwita balozi wake kutoka mjini Dublin baada ya Ireland kujiunga na Norway, Uhispania na Slovenia, katika hatua yao ya kulitambua taifa huru la Palestina.
Kwa upande wake Waziri mkuu wa Ireland Simon Harris ametaja kusikitishwa na uamuzi huo wa Israel:
” Inasikitisha sana kuona wamechukua uamuzi huo. Wana haki ya kuufunga ubalozi wao. Tutaendelea kushirikiana kwa njia za kidiplomasia, lakini hakuna mtu atakaeinyamazisha Ireland. Tunajua kutofautisha kati ya mema na mabaya. Tunathamini haki za binadamu na tunaheshimu sheria za kimataifa. Israel ina haki ya kujitetea na kuishi kwa amani na usalama lakini pia vitendo vya serikali ya Netanyahu kwa raia wasio na hatia huko Gaza na katika Ukingo wa Magharibi ni aibu na vinapaswa kulaaniwa na wote, ” alisisitiza Harris.
Soma pia: Jeshi la Israel limesema lishambulia kituo cha kuongioza vita cha Hamas huko Gaza
Wiki iliyopita, Baraza la mawaziri la Ireland liliamua kujiunga rasmi na Afrika Kusini katika kesi yake dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kesi ambayo inaishutumu Israel kwa kuendesha mauaji ya halaiki huko Gaza. Shutuma ambazo zimekuwa zikikanushwa na Israel.
Idadi ya vifo Gaza yapindukia watu 45,000
Maafisa wa afya wa Palestina wamesema mashambulizi mapya ya anga ya Israel katika maeneo mbalimbali huko Gaza yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 50. Shambulizi moja la anga lilipiga makazi ya wakimbizi wa ndani na kuwaua watu 17 wakiwemo wanawake na watoto huku shambulio jingine likiilenga shule ya Khalil Aweida katika mji wa Beit Hanoun na kuua watu wasiopungua 15.
Watu wengine kadhaa akiwemo ripota wa Al Jazeera Ahmed al-Lawh, wameuawa kufuatia shambulizi la Israel katika kambi ya Nuseirat katikati mwa Gaza. Watu wengine wamearifiwa kuuawa huko Khan Younis na hivyo kupelekea idadi ya vifo tangu Oktoba 7 mwaka jana kufikia watu 45,028.
Huku idadi hiyo ya vifo ikizidi kuongezeka, juhudi za kufikia makubaliano ya usitishaji mapigano zinazosimamiwa na Marekani, Misri na Qatar zimeshika kasi katika wiki za hivi karibuni baada ya mikwamo ya mara kwa mara. Wasuluhishi wamesema kumeshuhudiwa nia na utayari kutoka pande zote mbili ili kusitisha mapigano hayo.
(Vyanzo: DPA, RTR, AP, AFP)