Kwa nini Tanzania ina nafuu ya deni la taifa kuliko majirani zake

Dar es Salaam. Ni wazi kuwa Tanzania inakopa kiasi kikubwa kugharamia miradi ya miundombinu muhimu, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), lakini deni lake linaendelea kuwa himilivu ukilinganisha na nchi jirani, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni.

Hali hii inatokana na ukweli kuwa kiasi kikubwa cha mikopo ya Tanzania,  inatokana na mikopo ya taasisi za kimataifa, ambayo kwa kawaida huwa ya gharama nafuu ikilinganishwa na taasisi binafsi za kifedha.

Hii ni tofauti kabisa na baadhi ya nchi jirani, ambazo zimelazimika kuomba msamaha au likizo ya madeni kutokana na kukopa kwa kiasi kikubwa kutoka kwa wakopeshaji wa nchi mojamoja na wale wa kibiashara.

Kwa mfano, Juni 2023, Zambia ilikubaliana na wakopeshaji wake wa nchi moja moja kusimamisha upya deni la nje la dola bilioni 6.3, ikiwemo dola bilioni 4.1 ambazo inadaiwa na China.

Hali kama hiyo inaweza kuwa ndio iliyopo  nchini Kenya, ambapo deni la Taifa ni sawa na asilimia 70 ya Pato la Taifa (GDP), kiwango cha juu zaidi kwa kipindi cha miaka 20.

Kwa upande mwingine, asilimia 67 ya deni la nje la Tanzania linatokana na taasisi za kimataifa, kulingana na Ripoti ya Madeni ya Kimataifa 2024 ya Benki ya Dunia.

Benki ya Dunia imechangia asilimia 47 ya deni, huku Benki ya Maendeleo ya Afrika na mashirika mengine ya kimataifa yakichangia asilimia 13 na saba, mtawalia.

Kimsingi, wakopeshaji wa kimataifa hutoa mikopo yao kwa masharti nafuu, ambayo mara nyingi yanajumuisha viwango vya riba vya chini na vipindi virefu vya kulipa au vya neema.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Benki ya Dunia, ni asilimia 17 tu ya deni la Tanzania linatokana na taasisi za kibiashara za binafsi, huku wakopeshaji wa nchi moja moja kama China, India na Japan wakichangia asilimia 16 tu.

Kwa kulinganisha, asilimia 55 ya deni la Kenya linatokana na wakopeshaji wa kimataifa, huku wakopeshaji wa nchi moja moja wakichangia asilimia 23, ambapo asilimia 16 inadaiwa na China pekee.

Asilimia 22 ya deni limetokana na mikopo kutoka kwa wakopeshaji wa kibiashara.

Kwa upande wa Zambia, wakopeshaji wa kimataifa wanachangia asilimia 28 pekee ya deni lake.

Hali ni tofauti kabisa, kwani wakopeshaji binafsi, yakiwemo mashirika ya kibiashara na wamiliki wa dhamana za serikali,

wanachangia asilimia 42 ya deni la nchi hiyo, huku wakopeshaji wa nchi moja moja wakichangia asilimia 30, ambapo asilimia 22 inadaiwa na China pekee.

Kuhusu hali hiyo, Kamishna Msaidizi wa Usimamizi wa Madeni na Takwimu wa Wizara ya Fedha, Omary Khama, aliliambia gazeti dada la The Citizen kwamba Tanzania inakopa ili kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo kwa haraka.

“Kwa kuwa Tanzania haina rasilimali za ndani za kutosha kufadhili mipango yake yote ya maendeleo, inalazimika kuchukua mikopo yenye masharti nafuu, ambayo kwa kawaida huwa na vipindi virefu vya kulipa vya miaka 30 hadi 40 na viwango vya riba vya chini,” alisema.

Khama aliongeza kuwa Tanzania inategemea sana taasisi za kimataifa kwa mikopo hii kwa sababu huwa na masharti nafuu zaidi kuliko mikopo ya kibiashara, ambayo kwa kawaida huwa na vipindi vifupi vya ulipaji na viwango vya riba vya juu.

Alibainisha kuwa nchi hufanya tathmini za kila mwaka za uhimilivu wa madeni kuhakikisha kwamba mikopo yake inabaki kuwa himilivu.

Kwa kuwa sehemu kubwa ya mikopo ya Tanzania inatoka kwa taasisi kama Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika, ambazo hutoa mikopo ya muda mrefu yenye riba ya chini, deni la nchi linaendelea kuwa himilivu.

Jumla ya deni la taifa la Tanzania ilifikia dola bilioni 45.139 kufikia mwisho wa Oktoba 2024, kulingana na Ripoti ya Mapitio ya Kiuchumi ya kila Mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania ya Novemba 2024. Jumla ya deni la nje lilikuwa asilimia 73.1 ya deni lote.

Katika hali halisi, deni la nje lilifikia dola bilioni 32.977 kufikia mwisho wa Oktoba 2024.

Deni la nje linalodaiwa na serikali kuu liliendelea kuwa sehemu kubwa ya deni la nje, likichangia asilimia 77.2 ya deni lote la nje.

Dk Abel Kinyondo wa Chuo cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema hali ya deni la Tanzania ni thabiti ikipimwa kwa uwiano wa deni na Pato la Taifa (GDP).

Hata hivyo, alionya kwamba licha ya utulivu huu wa kiasi, rasilimali za ndani za nchi bado ni finyu.

“Ni muhimu kuchambua kwa makini aina za mikopo inayochukuliwa,” alisema Dk Kinyondo.

Ripoti ya Benki ya Dunia pia inaangazia mwenendo wa madeni duniani, ikibainisha kuwa mwaka 2023, nchi zinazoendelea zililipa jumla ya dola trilioni 1.4 kwa ajili ya huduma za madeni, ambapo ongezeko kubwa lilitokana na malipo ya riba.

Nchi nyingi, hasa zile zinazostahili msaada kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa (IDA), zimeona huduma za madeni zikiondoa rasilimali kutoka sekta muhimu kama afya na elimu.

Aidha, janga la Uviko-19 liliongeza mzigo wa madeni kwa nchi za kipato cha chini na cha kati, ambazo zililazimika kukopa sana kukabiliana na athari za kiuchumi za janga hilo.

Kufikia mwaka 2023, jumla ya deni la nchi hizo liliongezeka hadi dola trilioni 8.8, huku deni la nje kwa nchi maskini zaidi likiongezeka kwa asilimia 17.9 tangu 2020.

Mwaka 2023, asilimia 15 ya deni la nje la nchi za kipato cha chini na cha kati lilidaiwa na taasisi za kimataifa, ongezeko la asilimia nne kutoka viwango vya kabla ya janga.

Ingawa ukopaji wa sekta binafsi umeanza kurejea, utolewaji wa deni kutoka kwa wamiliki wa dhamana bado ni changamoto kwa nchi nyingi.

Kwa kulinganisha, mkakati wa Tanzania wa kukopa kutoka taasisi za kimataifa umesaidia kuhimili mzigo wake wa madeni kwa ufanisi zaidi kuliko mataifa mengi yanayokumbwa na matatizo makubwa ya madeni

Related Posts