Leverkusen yarejea katika mbio za ubingwa – DW – 16.12.2024

Bayern Munich watamaliza wakiwa kileleni isipokuwa wakitizama nyuma yao wanawaona mabingwa watetezi Bayer Leverkusen. Bayern wanaongoza na pointi 33, nne mbele ya nambari mbili Levekusen na kwa kutegemea jinsi matokeo yatakavyokuwa wikiendi nijayo, huenda pengo hilo likapungua hadi pointi moja. Matokeo ya mwishoni mwa wiki yaliwafaidi Leverkusen.

Vinara Bayern walipoteza pointi tatu ikiwa ni kichapo chao cha kwanza cha msimu chini ya kocha Vincent Kompany. Makosa katika safu ya ulinzi yalichangia katika kichapo cha 2 – 1 mikononi mwa Mainz. Bayern wameshinda mechi moja tu kati ya zao tatu za mwisho. “Hongera kwa kocha mwenzangu na Mainz kwa pointi tatu na ushindi. Na nadhani, tulicheza dhidi ya timu yenye kujiamini sana na nadhani timu ambayo ilikuwa imejiandaa kupambana kila dakika. Kwa upande wetu, sidhani kulikuwa na ukosefu wa ari ya kupambana. Nadhani nasi pia tulipambana kadri ya uwezo wetu.”

Bundesliga FSV Mainz 05 - FC Bayern München
Mainz waliwapa Bayern kichapo cha kwanza katika Bundesliga chini ya kocha Vincent KompanyPicha: Thomas Frey/IMAGO

Hayo yametokea wakati mshambuliaji wao matata Harry Kane akiwa mkekani. Kompany hata hivyo amesema Kane anaweza kurudi dimbani katika mechi ijayo. Leverkusen yake Xabi Alonso ilitumia vyema fursa hiyo kwa kupungua mwanya wa Bayern na kuwasha tena moto wao wa kuwania taji. Waliwazaba Augsburg 2 – 0 na kuruka hadi nafasi ya pili, pointi mbili mbele ya nambari tatu Frankfurt ambao walicharazwa 2 – 1 na RB Leipzig. Alipoulizwa kama wamerejea kwenye mawindo ya ubingwa, Alonso alijibu: “Hapana, hapana, bado. Tunafanya kivyetu. Hilo ndilo jambo muhimu zaidi.” Najua. Muonekano wa Jedwali mwishoni mwa Desemba, sio muhimu sana. Bado kuna mechi nyingi za kucheza. “

Sasa mambo yatapamba moto wikiendi ijayo, Leverkusen wakiwinda ushindi wao wa tano mfululizo nyumbani dhidi ya Freiburg ambao wako nafasi ya tano. Nao Bayern watakuwa na kibarua kikali dhidi ya RB Leipzig. Kocha wa Bayern Kompany anasema baada ya kichapo cha Mainz, watakuwa tayari kupambana tena. “Tutatumia kichapo hicho cha leo kuwasha moto katika siku chache zijazo kuelekea mchezo wetu wa Ijumaa, kwa sababu ndio wakati pekee tunaweza kutoa jibu.”

Afp, dpa, ap, reuters

Related Posts