Lissu adai kuwasilisha majina ya waliopenyezewa fedha za uchaguzi Chadema

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu amesema ameshapeleka ushahidi kuhusu madai ya rushwa ndani ya chama hicho kwenye vikao halali, hivyo anatarajia utekelezaji.

Lissu aliyetangaza kugombea uenyekiti wa chama hicho Desemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam, amesema mambo aliyoyataja kama changamoto atakazozishughulikia ndio ajenda zake za uchaguzi.

Kauli ya Lissu imekuja saa chache tangu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuwaeleza waandishi wa habari leo Jumatatu, Desemba 16, 2024 akiwataka viongozi na wanachama wenye malalamiko ya kimaadili wayapeleke na sio kutoa malalamiko ya jumlajumla.

“Kuhusu tuhuma ambazo makamu (Lissu) amezitoa kuhusu uadilifu nisisitize kwa nafasi yangu ya utendaji mkuu wa chama, ikiwa kuna kiongozi au mtu yoyote wa Chadema ana tuhuma dhidi ya yoyote aziwasilishe ili zishughulikiwe kwa mujibu wa Katiba, itifaki na maadili ya chama na sio kutoa tuhuma za jumlajumla bila kusema hapa kuna huyu anatuhumiwa na huyu na hili na hili.

“Tukipata tuhuma zenye ushahidi zitapelekwa kwenye kamati kuu ya chama ambayo itaamua kushughulika nayo au kupeleka Kamati ya Maadili,” alisema Mnyika.

Hata hivyo, akizungumza katika mahojiano na Mwananchi leo Desemba 16, 2024 Lissu amesema baada ya kutoa madai ya kuwepo fedha zilizopenyeshwa ndani ya chama hicho, aliitwa kwenye kikao cha kamati kuu na aliwasilisha ushahidi wake.

“Nilizungumza hiyo habari ya pesa chafu kwenye mkutano wa hadhara Iringa (Mei 2, 2024). Kabla ya kuzungumza kwenye mkutano huo, nilikuwa nimewaandikia wajumbe wote kwenye kamati kuu nikiyalalamikia hayo masuala.

“Badala yake nikatengenezewa kikao cha kamati kuu nikazungumze na kutaja majina, niliyataja yote niliyoyajua. Hawajatoa hiyo taarifa mpaka leo,” amesema Lissu.

Amesisitiza kuwa matumizi ya fedha katika chaguzi za chama hicho yapo na alishayatolea taarifa kwenye chama.

“Yeyote anayefuatilia chaguzi za chama, hii habari ya matumizi ya fedha kuhonga wajumbe iko kila mahali, hawataki tu kusema,” amesema.

Lissu amekifananisha kikao hicho na halmashauri kuu ya CCM iliyoketi mwaka 1984 na kumng’oa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe.

“Hicho kikao kilikuwa, unafahamu historia ya Aboud Jumbe alivyong’olewa? Kilikuwa kikao cha aina hiyo. Nilipowapa hayo majina hiyo ajenda ilikufa, kwa hiyo mtu anayesema natuhumu bila majina, muulizeni katibu mkuu anayekaa na nyaraka za chama,” amesema.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alipotafutwa kwa simu hakupokea.

Kuhusu ajenda ya ukomo wa madaraka, Lissu amesema alishaisema kwenye kikaco cha chama mwaka 2015 wakati wa uteuzi wa wabunge wa viti maalumu.

“Kuhusu ukomo wa madaraka kwa viti maalumu hilo suala nilizungumza mwaka 2015 wakati tunateua wabunge wa viti maalumu waliotokana na uchaguzi wa mwaka huo, wakasema hatuwezi kuanza suala hilo mwaka huo tutalianza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Amesisitiza kuwa hilo so jambo jipya kwenye chama, huku akitaja baadhi ya viongozi aliodai waliwahi pia kulizungumzia.

“Atakayesema kuweka ukomo wa madaraka ni jambo jipya atakuwa sijui ana maana gani. Kama huu sio wakati sahihi wa mimi kulizungumza sasa hivi ni wakati gani? Hizo ni ajenda zangu. Hoja kwamba hatukuzungumza mapema ina maana kama hatukuzungumza ndio hayapaswi kushughulikiwa? Kama hatukuzungumza huu ndio wakati wa kushughulikiwa,” amesema.

Ameendelea kusema hata kama mambo hayo hayakuzungumzwa kwenye vikao awali, milango bado haijafungwa na hiyo ndio ajenda yake ya sasa.

Akizungumzia maelezo yake kuhusu mfumo wa uchaguzi, Lissu amesema kwa kiasi kikubwa utaratibu uliowekwa katika katiba ya Chadema haujafuatwa.

“Tumeacha kufuata katiba, yote yanayofanyika kwenye uchaguzi yameacha kabisa katiba. Kwa mfano usimamizi wa uchaguzi, wanaotakiwa kusimamia uchaguzi wa ngazi ya vijiji ni kata, wa ngazi ya kata ni wilaya au mkoa, wa ngazi ya mkoa ni kanda na kanda ni ngazi ya taifa. Kwa hiyo turudi kwenye katiba ya chama,” amesema.

Related Posts