Mshambuliaji wa Atalanta na timu ya taifa ya Nigeria, Ademola Lookmann leo, Desemba 16, 2024 ameibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora Afrika 2024 ya shirikisho la mpira wa miguu Afrika (Caf) katika hafla iliyofanyika Marrakech, Morocco.
Lookman ambaye amekuwa na nyakati bora akiwa na klabu yake ya Atalanta inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’, ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda Achraf Hakimi, Serhou Guirassy, Simon Adingra na Ronwen Williams.
Akiwa na Atalanta, Lookman ameiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Uefa Europa League ambapo alifunga mabao matatu yaliyoipa ushindi timu yake katika mechi ya fainali dhidi ya Bayer Leverkusen.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Everton, alikuwa na mchango kwa timu ya taifa ya Nigeria kwa kuiongoza kufika fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika mwaka huu huko Ivory Coast, alifunga mabao yote katika mechi ambayo Nigteria ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Cameroon kwenye hatua ya 16 bora lakini pia alifunga bao pekee la ushindi katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Angola.
Mchezaji bora Afrika kwa wanawake ni Barbara Banda wa Zambia na klabu ya Orlando Pride akiwashinda Chiamaka Nnadozie na Sanaa MsSoudy.
Ronwen Williams wa Afrika Kusini na Mamelodi Sundowns, alishinda tuzo mbili ambazo ni mchezaji bora Afrika wa mashindano ya ndani ya Afrika na ile ya kipa bora Afrika huku Chiamaka Nnadozie akishinda tuzo ya kipa bora Afrika kwa wanawake namchezaji bora Afrika wa ndani ni Sanaa MsSoudy.
Lamine Camara wa Senegal ameshinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi wanaume n a upande wa wanawake ameshinda Doha El Madani wa Morocco.
Kocha bora Afrika kwa wanaume ni Emerse Fae anayeinoa Ivory Coast na kwa upande wa soka la wanawake ni Lamia Boumehdi anayeinoa timu ya wanawake ya TP Mazembe.
Timu bora ya taifa ya wanaume ni Ivory Coast na kwa upande wa wanawake ni Nigeria na kwa upande wa klabu, timu iliyoshinda kwa wanaume ni Al Ahly na wanawake ni TP Mazembe.
Cristovao Mabululu ameibuka mshindi wa tuzo ya goli bora la mwaka huku pia Caf ikiwazadia Rais wa Misri, Abdelfattah El-Sisi na Rais wa Cameroon, Paul Biya kwa mchango wao kwa maendeleo ya soka kwenye nchi zao.
Kwa mara ya kwanza, Caf ilitoa tuzo za marefa bora ambapo kwa wanaume ameshinda Ibrahim Mutaz wa Libya na kwa wanawake ameshinda Bouchra Karboubi wa Morocco.
Diana Chikotesha ameshinda tuzo ya refa bora msaidizi wa kike na refa bora msaidizi wa kiume ni Elvis Guy Noupue Nguegoue.