Maajabu chemichemi ya Berabara Kondoa

Kondoa. Upo msemo wa Kiswahili usemao: ‘Tembea uone’. Msemo huu unamaanisha kuwa kwa kutembea maeneo mbalimbali, unaweza kuona, kujifunza na kujua masuala mengi.

Ukweli wa msemo huo unadhihirika ukitembelea katika Kijiji cha Berabera, kata ya Kikilo, Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma ambapo unakutana na chemichemi ya asili iliyotambulika miaka 200 iliyopita.

Mfuniko wa kisima ukiwa pembeni ya kisima. Mfuniko huo huwa ukitoka wenyewe kisimani.

Chemchemi hiyo inapatikana umbali wa kilomita 207.9 kutoka Jiji la Dodoma na kilometa 13.7 kutoka makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa iliyopo eneo la Bukulu.

Upekee wa chemichemi hiyo, ambayo inategemewa kwa kuwa ndio chanzo kikuu cha maji katika eneo la Kondoa Mjini, unatokana maajabu unayokutana nayo katika eneo hilo ambacho pia ni kivutio cha utalii.

Kwa mujibu wa tovuti ya Hamashauri ya Mji wa Kondoa, chemichemi hiyo  inachangia katika mfumo ikolojia wa mto Bubu,  unaoanzia Mkoa wa Manyara na mtiririko wake wa maji kwenda hadi Bahari ya Hindi kupitia halmashauri za Kondoa Mjini, Chemba, Bahi, Mpwapwa, Kilosa hadi  Mto wami. 

Jina la kijiji hicho cha Berabera limetokana na tabia ya maji ya chemichemi hiyo ambayo yalikuwa yakitoka kwa kuruka ruka juu ardhi,  kutetemeka au kucheza cheza na kwa wenyeji wa asili ‘Kibarabaig’ kitendo hicho kwa kilugha chao kinaitwa birabira.

Inaelezwa kuwa  baada ya jamii ya Kirangi kuingia eneo hilo, walishindwa kutamka ‘birabira’ na kutamka berabera ndipo kijiji hicho kikaitwa berabera.

Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kondoa (KONDUWASA), Boniface Mwamkinga anasema chemichemi hiyo ya asili ilianza kutumiwa na wakazi kuchota maji tangu mwaka 1943.

Mwonekano wa kisima kwa ndani

Hata hivyo, mwaka 1980, Serikali ijenga miundombinu na kusambaza huduma kwa wakazi wa mji huo na baadaye kufanya marekebisho mengine mwaka 2007.

 Mhandisi huyo anasema kwa sasa chemichemi hiyo inazalisha lita milioni 3.2 za maji kwa siku huku ikiwahudumia wakazi wapato 39,000 ambao wanaendelea kuongezeka kila siku kutokana na kukua kwa mji huo.

“Kwa muda mrefu sana chanzo hakipungui ingawa kuna mabadiliko ya nchi na mvua kutokana na ulinzi uliofanyika wa kupanda miti, kulindwa kwa wakati huu na kuitunza, tunatarajia itatoa huduma miaka na miaka,”anasema.

Mwamkinga anasema chemichemi hiyo imeambatana na historia kubwa ambapo mfuniko wa chemchem huo,  ambao ni wa chuma umeshindikana kukaa katika eneo la juu.

Huku akionyesha mfuniko huo uliotengenezwa kwa vyuma vitupu, ambao kwa maelezo ya aliowakuta,  anasema kila wanapouweka mfuniko huo, wanapoamka asubuhi wanaukuta pembezoni mwa kisima ukiwa umeondolewa.

Anasema kutokana na mfuniko huo kuondoka mara nyingi, iliwalazimu kukiacha wazi kwa juu.

“Wazee wa eneo hili wanasimulia kuwa kuna mzungu pia alizamia katika chemchem hii kwenda kukagua kina lakini ilishindikana, alitoweka kabisa na alishindwa kurejea duniani hadi hivi leo,”anasema.

Kwa mujibu wa tovuti ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa, ukifika katika eneo la chemchem utakutana na maajabu ya tope la volcano na kuwa eneo hilo si rahisi mtu yeyote kwenda katika eneo hilo kutokana na uwezo wake wa kumeza vitu au kitu chochote kitakachoingia katika tope.

“Kwa maelezo ya wazee wa mila ukiingia eneo hilo hata uvutwe na kitu gani huwezi kutolewa kulingana na nguvu iliyopo katika eneo lenye tope,”inasema sehemu ya tovuti hiyo.

Alipoulizwa kwa nini uchafu hauingii katika chemchem hiyo, Mwamkinga anasema hiyo ni moja ya maajabu ya chemchem hiyo licha ya uwazi uliopo juu na miti mingi inayozunguka lakini hakuna uchafu unaoingia kwenye chanzo hicho.

Anasema muundo wa chemchem hiyo pia unasaidia majani na uchafu unaotoka katika miti hiyo yasiingie ndani ya chanzo hicho cha maji ambapo ndani yake kuna umbo la tembo.

Anasema wamekuwa wakipata watalii wengi kutoka mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Arusha kushuhudia maajabu ya kisima hicho ambacho hutoa maji ya moto.

“Nawashauri wakazi hawa walipe bili za maji na pia watunze mazingira ya eneo hili kwa manufaa yao, kizazi cha sasa na kizazi cha baadaye,”anasema.

Anasema kwa mwezi wanapokea kati ya watalii watano hadi sita wa kutoka nje ya nchi,  huku Watanzania kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiwa kati ya 20 hadi 40. 

Naye mlinzi wa chemchem hiyo ambaye amekuwa hapo tangu mwaka 2015, Salim Juma anasema chemchem hiyo ilitanuka baada ya tembo kuteleza na kutumbukia alipopita na wenzake  kwenye eneo hilo kunywa maji.

“Baada ya kuzama kwa tembo, walikaa kwa muda, akaja mtafiti kupima urefu wa chemchem lakini alipoingia hadi leo hajafanikiwa kurejea. Hivyo hadi leo chemchem hii haijulikani ina kina gani,”anasema.

Juma anasema nyakati za usiku kuanzia saa 4.00 hadi 11.00 alfajiri kuna nyoka watatu ambao hulinda chemchem nyakati hizo kwa kulala juu ya miti inayoizunguka.

“Nyoka hao wanaelekeza macho yao barabarani na mmoja kazi yake ni kuzunguka fance (uzio) wa chemchem hiyo na mwingine hukaa katikati ya geti. Nilipofika na kukutana na hali hii niliogopa sana lakini baada ya muda nilianza kuzoea,”anasema.

Anasema licha ya nyoka hao pia kuna paka ambaye hukaa katika geti katika muda huo akilinda kwenye eneo hilo lakini kunapokucha hutokomea kusikojulikana.

Juma anasema pia, nyakati za saa 10:00 jioni huwa kuna  kelele za sauti ya ngoma za asili zinazopigwa katika msitu unaozunguka chemchem hiyo na watu wasiojulikana.

“Ngoma hizi ukizifuata huko sauti inayotokea zinahama na kusikika upande mwingine. Lakini wenyeji wanasema ni mizimu ndio inayopiga ngoma hizo ambazo kama ni mara yako ya kwanza ni lazima uogope kwa sababu humuoni anayepiga lakini milio unasikia,”anasema Juma.

 Mlinzi huyo anasema unapofika katika eneo hilo nyakati za usiku, unakutana na giza nene ambalo linaongeza hofu kwa mtu anayekuwepo katika eneo hilo.

 Alipoulizwa kama wenyeji wanafika kwa ajili ya kutambika, Juma anasema awali kabla ya kujengewa uzio na kuanza kutumika kama chanzo kikuu cha maji, wenyeji walikuwa wakikitumia kutambika mizimu.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Jimbo la Kondoa, Eliazer Mbwambo anasema chemchem hiyo ni utalii wa ndani na kuwashauri Watanzania kupenda kutembelea vivutio hivyo, badala ya kusubiri watu wa kutoka nje ya nchi waje kuwahadithia.

“Tuendeleze utalii wa kuja kuangalia vivutio hivi vya utalii ambavyo vipo ndani ya nchi yetu, mkoa wetu wa Dodoma. Ninawaalika watu wengine waje waone maajabu ya maji yanayochemka ambayo ni ya moto. Kwa kweli ni mahali ambapo utapenda kuendelea kuangalia,”anasema.

Anasema Watanzania hawana haja ya kuhofia kiingilio cha kwenda kutazama kivutio hicho kwa sababu kila mtu anaweza kumudu Sh1,000.

Mtalii mwingine kutoka Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Esther Nembela anasema alikuwa anasikia uwepo wa chemchem hiyo ya ajabu ambayo alitamani kufika kujionea mwenyewe maajabu yaliyopo.

“Nilipata maelekezo na sasa nimefika, kwa kweli nimefurahia nawaasa wenzangu karibuni Wilaya ya Kondoa, mje mshuhudie chemchem hii. Nimeona kina muundo wa umbo la tembo kwa kweli inavutia sana,”anasema.

Related Posts