Dar es Salaam. Hitaji la Katiba mpya, maboresho ya mfumo wa elimu na mbinu za kutatua migogoro ya ardhi, ni mambo matatu yaliyosisitizwa na wahariri wa vyombo vya habari kwenye majdala wa uhakiki wa rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Maoni hayo yametolewa katika kikao cha kuhakiki rasimu ya dira hiyo kati ya Tume ya Taifa ya Mipango na wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari leo Jumatatu, Desemba 16, 2024 jijini Dar es Salaam.
Akitoa maoni yake katika mjadala huo, mmiliki mwenza wa gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton amesema dira hiyo ina mambo mengi, lakini inahitaji kibali, yaani Katiba mpya.
“Haya mtatekekezaje wakati Katiba ambayo ni muongozo mama haijatupa tunakwenda wapi? Angalieni mjue mnaweka wapi kama 2028 au 2030 muweke ili itubane huko mbele,” amesema.
Manyerere amesema kitendo cha kufanya mambo kwa huruma ya kiongozi aliyepo madarakani haiwezi kuifikisha Tanzania 2050.
“Dira ni muhimu izungumze katiba itapatikana lini bila kuona aibu,” amesema.
Kwa upande wake, mhariri wa gazeti la Raia Mwema, Joseph Kulangwa amesema ni muhimu kuangalia katika kipindi kifupi kuwe na Katiba mpya.
“Tusipotekeleza ambacho Watanzania wengi wanataka sasa hivi ambayo ni Katiba mpya, ni maaandalizi ya kuwa na nadharia zisizotekelezeka, kwani vurugu zinaweza kujitokeza,” amesema.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema suala la mabadiliko ya Katiba lipo kwenye rasimu ya dira hiyo, lakini utekelezaji ni hatua ya baadaye na sasa ni kipindi cha ndoto.
Profesa Mkumbo amesema ndani ya dira hiyo kuna shabaha ya Tanzania kuwa ni Taifa la kidemokrasia linaloongozwa na katiba imara inayoakisi muafaka wa kitaifa, taasisi madhubuti za umma na mfumo wa vyama vingi vya siasa.
“Kwenye dira hayo yanatosha, kwenye mpango huko ndiko kutaelezwa hili litekelezwe lini, nao wadau wataitwa kwenda kujadiliana kuhusu hilo jambo,” amesema.
Akizungumzia mfumo wa elimu nchini, Jesse Kwayu wa Media Brain amesema katika mambo Tanzania inayafanyia mchezo ni sekta ya elimu, akisema imeonekana kila waziri wa sekta ya elimu anayeingia anakuwa na ndoto zake kwenye sekta hiyo.
“Huyu anaingia anafuta kilimo, anafuta nini hatuna kitu ambacho yeyote kitatuelekeza, kila anayeshika nafasi ya utawala tutataka afuate hayo bila kutekeleza kufanya hivyo tutapata shida,” amesema.
Amegusia pia migogoro ya ardhi akisema sekta hiyo ina changamoto nyingi, lakini ipo hofu ya kusema ni namna gani zitashughulikiwa.
“Mfano tuseme ifikapo 2050 kila kipande cha ardhi ya nchi hii iwe imepimwa na iwe na karatasi yake ili kutatua migogoro, tusipofanya hivyo tunaliachia eneo hilo kuendelea kuwa na migogoro baadaye, “amesema.
Akihitimisha mkutano huo, Profesa Kitila amesema watazingatia maoni hayo na yapo mambo mapya yaliyoibuka, ikiwemo suala la mawasiliano kwa kuwa ni nyenzo muhimu na wasipozingatia litawaletea shida.
“Kila baada ya miaka mitano kutakuwa na mapitio ya utekelezaji wa dira, hivyo kama yapo mambo yamejitokeza lazima yataingizwa,”amesema.