Mashine sita zinatua Tabora United

KATIKA kuimarisha zaidi kikosi chake, kocha mkuu wa Tabora United, Anicet Kiazmak ameagiza mashine sita kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo ili kuongeza nguvu katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Kikosi hicho ambacho kilikuwa chini ya Mkenya Francis Kimanzi, hakikuanza msimu vizuri lakini gari limekuja kuchanganya baada ya ujio wa Anicet huku kocha huyo akiweka wazi kwamba anataka mshambuliaji mmoja, viungo watatu, beki mmoja na kipa.

Timu hiyo iliyocheza mechi 14 ikibakiwa na moja kukamilisha mzunguko wa kwanza, inashika nafasi ya tano, ikiwa imeshinda michezo saba, sare tatu na kupoteza minne ikikusanya alama 24.

Taarifa za ndani zinasema kwamba kocha huyo amezungumza na mabosi wa klabu hiyo mapema na kuwapa mipango yake kabla ya mzunguko wa pili haujaanza.

“Kocha katika ripoti yake anataka mashine mpya sita ambapo ni mshambuliaji mmoja, viungo watatu, beki mmoja na kipa ambao wataongeza nguvu katika raundi ya pili ya ligi ili kujihakikishia kusalia katika nafasi nzuri zaidi ya hapa timu ilipo sasa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema, anaiandaa timu yake kufanya vizuri huku kwa sasa akiona bado haijafika kwenye kiwango anachotaka.

Alisema kuwa, anataka timu yake itengeneze nafasi nyingi na kuzitumia lakini pia kucheza mpira wa kasi zaidi.

“Nataka kikosi kicheze soka la ushindani hasa mpira wa kasi na kila mchezaji kuwa makini na eneo lake ili kuwazuia wapinzani kila pande wasilete madhara.

“Licha ya kuwa tunajitahidi kufanya vizuri lakini kwangu naona kuna kazi kubwa ya ziada kuhakikisha malengo ya timu, wachezaji na yangu yanatimia,” alisema kocha huyo raia wa DR Congo.

Related Posts