Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amekanusha madai ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu yakiwamo ya ukosefu wa uadilifu na mfumo mbovu wa fedha, akitaka wanachama wenye malalamiko kama hayo kuyawasilisha kupitia njia rasmi za chama.
Akitangaza nia yake ya kuwania uenyekiti wa Chadema jijini Dar es Salaam Desemba 12, Lissu alieleza haja ya kurekebisha mfumo wa fedha, mfumo wa uchaguzi, kuweka ukomo wa uongozi, kuwa ajenda zake atakaposhinda katika kinyang’anyiro hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Desemba 16, jijini Dar es Salaam, Mnyika amefafanua kuwa Chadema ina utaratibu wa kushughulikia tuhuma, kupitia vikao vya kikatiba vya chama, hususan Kamati Kuu kwa ngazi ya taifa.
“Tuhuma yoyote inayohusiana na ngazi ya kitaifa lazima ifikishwe Kamati Kuu, na mpaka sasa, kama Katibu Mkuu, sijawahi kuletewa jambo lolote rasmi la aina hiyo.
“Nisisitize kwamba, ikiwa kuna kiongozi yeyote au mwanachama wa Chadema mwenye tuhuma dhidi ya yeyote, azilete kwa mujibu wa Katiba, itifaki, na maadili ya chama. Tusikubali kutoa tuhuma za jumla bila kueleza bayana nani anatuhumiwa, kwa nini, na kwa ushahidi gani,” amesema Mnyika.
Kauli ya Mnyika inakuja wakati kukiwa na joto la uchaguzi hasa kwa ngazi ya Taifa, ambapo Lissu ametangaza kugombea uenyekiti.
Japo Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe hajatangaza nia ya kugombea tena, vita hiyo inatajwa kumwandama hasa baada ya tangazo la Lissu.
Awali akitangaza ufunguzi wa pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu za uchaguzi mkuu wa chama hicho kuanzia Desemba 17, 2024 hadi Januari 5, 2025, Mnyika amesema nafasi zitakazogombea ni pamoja na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na mabaraza kwa ngazi ya taifa.
Amesema mkutano mkuu unatarajiwa kufanyika Januari 21, 2025 ukitanguliwa na mikutano ya mabaraza ya Vijana (Bavicha), wazee (Bazecha) na wanawake (Bawacha) kwa siku tofauti.
Akizungumza Dar es Salaam leo Desemba 16,2025 kwenye mkutano wake na vyombo vya habari, Mnyika ametaja muda wa mwisho wa kurejesha fomu ni 10 jioni Januari 5,2025, huku akieleza gharama za uchukuaji fomu zinatofautiana kulingana na nafasi anayoomba mgombea.
“Fomu zitaanza kutolewa kesho, gharama za fomu zinazingatia hali halisi ya kimaisha na mara ya mwisho zilipitiwa kwenye mkutano mkuu tangu mwaka 2019 na havijabadilishwa.
“Uchaguzi utakaofanyika Januari 2025, fomu za kuomba uongozi zinapatikana makao makuu ya chama, makao makuu ya mabaraza, ofisi za kanda, ofisi za chama mikoa na wilaya,” amesema.
Mnyika amesema fomu hizo zitaanza kutolewa kuanzia kesho Desemba 17, 2024 na mwisho wa kurejesha fomu Januari tano 2025 majira ya saa 10 jioni ofisi za chama hicho Mikocheni au ofisi za kanda anakotoka mgombea.
Pia kwa wanaogombea katika mabaraza ya vijana, wanawake na wazee watatakiwa kurejesha fomu zao kwenye ofisi za mabaraza hayo zilizopo Mtaa wa Ufipa Halmashauri ya Kinondoni au ofisi za kanda anakotoka mgombea husika.
“Gharama ya fomu itategemea na nafasi anayogombea na atatakiwa kuambatanisha risiti ya malipo katika fomu yake na malipo yanapaswa kulipwa kwenye akaunti ya chama au kwa kila baraza ambalo mwanachama anagombea na namba zimetajwa kwenye kila fomu ya mgombea,” amesema.
Mnyika ametaja gharama za uchukuaji fomu kwa nafasi zinawaniwa Mwenyekiti wa Taifa gharama ya fomu ni Sh1.5 milioni, makamu mwenyekiti Bara Sh750,000.
“makamu mwenyekiti Zanzibar Sh 750,000, wajumbe nane wa Kamati Kuu kati yao watatu wanaume,watatu wanawake kutoka Tanzania Bara angalau mmoja awe mtu anayeishi na ulemavu na mwanamke mmoja na mwanaume kutoka Zanzibar, gharama zao za fomu ni Sh300,000” amesema.