Mwanjala alia na soka la Mbeya, atoa matumaini kwa Yanga na Simba Caf

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Mbeya (Mrefa), Elias Mwanjala, ameonyesha kusikitishwa na timu alizoziacha kwenye ramani za mpira kupotea na zilizopo kuchechemea.

Mwanjala aliongoza Mrefa kwa miaka nane tangu, 2012 hadi 2020 ambapo alienguliwa katika nafasi hiyo na kufungiwa miaka miwili kwa kukiuka katiba ya Chama hicho kwa kugombea vipindi vitatu kinyume na kanuni.

Katika kipindi alichoongoza, Mwanjala aliziacha Tukuyu Stars ikishiriki Ligi Daraja la Pili ambayo sasa inaitwa First League na Boma FC ikicheza Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship), zote hazipo kwenye ligi hizo wakati Mbeya Kwanza na Mbeya City zilikuwa Ligi Kuu Bara na sasa zinashiriki Championship.

Hata hivyo, Mwanaspoti inafahamu wazi kuwa Mwanjala tayari amechukua fomu za kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Mrefa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Januari 19, 2025.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwanjala amesema masikitiko yake ni kuona soka la mkoa huo likishuka tofauti na kipindi chake ambapo Mbeya ilikuwa na heshima kubwa nchini kwenye kandanda.

Amesema matarajio yake iwapo atarejea katika uongozi ni kurejesha hadhi na heshima ya mkoa huo kwa timu kuonyesha ushindani na kutengeneza muunganiko baina ya mashabiki na wadau wa soka.

“Nataka soka la vijana na wanawake lichezwe, zile ndondo ziwekwe kwenye mkakati kuibua vipaji, kuwepo na muamko wa mashabiki kuzipenda timu zao na kuzipa sapoti uwanjani.

“Tatizo kubwa ni viongozi wanafikiria kulipwa na mpira badala ya wao mpira kuwategemea, sifurahishwi na matokeo ya timu zetu Prisons na KenGold japokuwa zinaweza kufanya vizuri kama zitatumia vyema dirisha dogo la usajili,” amesema Mwanjala.

Kuhusu Simba na Yanga kutoboa michuano ya kimataifa, mdau huyo wa soka na mwanasheria, amesema timu hizo zinaweza kufuzu robo fainali.

“Tumpe maua yake Kibu Denis kwa kazi nzuri aliyofanya jana, Simba ina nafasi kubwa ukilinganisha na Yanga, ila kwa mtazamo zote zinaweza kwenda robo fainali,” amesema shabiki huyo lialia wa Yanga.

Related Posts