Dar es Salaam. Mfanyabiashara Daisle Simon Ulomi, aliyepotea tangu Desemba 11, 2024 amekutwa amekufa na mwili wake kukutwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.
Ulomi aliyekuwa akifanya biashara za fedha za mitandao ya simu maeneo yaa Sinza Kijiweni na Mwenge alipotea tangu 11 Desemba 2024.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro zinaendelea, baada ya simu zake kuita bila kupokelewa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Desemba 16, 2024 baba mkwe wa Ulomi, Japhet Munisi amesema alipigiwa simu leo asubuhi na mke wa marehemu, akimjulisha kuwa amepata taarifa kuwa mwili wa mumewe uko hospitali.
“Baada ya kupata taarifa hiyo nilifika Hospitali ya Mwananyamala na kukuta askari wakiwa eneo la kuhifadhia maiti. Niliwauliza wahudumu pale hawakutaka kunieleza lolote.
“Niliwauliza askari waliokuwepo eneo hilo nao wakasema wanafanya uchunguzi kwanza ndipo watatoa taarira,” amesema Munisi.
Amesema kwa sasa wanandugu wanakusanyika Mikocheni kupinga taratibu za mazishi.
Taarifa zilizopatikana mitandaoni, zimeeleza kuwa siku hiyo (Desemba 11), Ulomi aliondoka Sinza Kijiweni saa 6 mchana, aliaga kuwa anakwenda Mbangala, bandari kavu kukagua kontena lake baada ya kuitwa na watu waliodai walikuwa wanashughulikia kulitoa bandarini.
Taarifa hiyo inasema aliondoka ofisini kwake akiwa na usafiri wa pikipiki akiendesha mwenyewe na tangu siku hiyo hakuonekana tena hadi mwili wake ulipopatikana akiwa amefariki.