SERIKALI ya Tanzania kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha mpango wa kuunda timu maalum inayokusudia kufanya uchambuzi na uchunguzi wa kina kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji nchi nzima. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea)
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuanzisha timu hiyo itakayojumuisha watoa huduma za msaada wa kisheria, ikiongozwa na Wizara kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign, Tume ya Haki za Binadamu, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Tanganyika Law Society (TLS), pamoja na Mahakama.
Waziri Dk. Ndumbaro ametoa agizo hilo leo, tarehe 16 Desemba 2024, Makao Makuu ya Wizara, Mtumba Jijini Dodoma wakati akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, ambaye sasa amehamishiwa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Amesema, “Ile Mobile Court tunahitaji, twende kila kwenye migogoro ya wakulima na wafugaji, tuweke kambi pale, tunamaliza tunakwenda sehemu nyingine, Haiwezekani nchi ya Amani kama Tanzania alafu migogoro haiishi, tusiidharau kwa sababu imekuwa donda ndugu sasa.”
Waziri Ndumbaro amesisitiza umuhimu wa kutatua migogoro hiyo kwa haraka ili kudumisha amani na utulivu wa kijamii, na kuonyesha kuwa migogoro hii imekuwa ni changamoto sugu katika jamii.
Kwa upande wake, Prof. Kabudi ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumwamini na kumuweka katika nafasi hiyo, akiahidi kuendelea kuchangia kwa bidii katika nafasi yake mpya.
Kwa hatua hiyo Serikali inaendelea kutafuta suluhu za kudumu katika migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiathiri uhusiano wa kijamii na uchumi kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali ya nchi.