Ni mwisho wa CUF? | Mwananchi

Dar es Salaam. Mgogoro unaofukuta ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kinafanya uchaguzi wa kanda kwa sasa unahusishwa na ukomo wa madaraka.

Ukomo huo unaozua mgogoro ni wa nafasi ya mwenyekiti taifa ambayo kwa sasa inashikiliwa na Freeman Mbowe ambaye amedumu kwa miaka 20. Hajaweka wazi iwapo atajitosa kutetea wadhifa huo kwenye uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika baadaye mwakani.

Wakati Chadema kukiwa na sintofahamu baada ya Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu kutangaza nia kuwania nafasi hiyo, ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) nako kuna fukuto la chini kwa chini, Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba akitajwa kuwa miongoni mwa wanaowania nafasi hiyo kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 18 na 19, 2024.

Profesa Lipumba, ambaye amekalia kiti cha uenyekiti wa CUF tangu mwaka 1999 kama atashinda ataweka rekodi ya kukiongoza chama hicho kwa miaka 30.

Licha ya kwamba, si dhambi kwa kiongozi kuongoza muda mrefu kwa mujibu wa katiba za vyama hivyo, kudumu kwao madarakani kunaibua minong’ono miongoni mwa wanachama na kutengeneza makundi kama ilivyo ndani ya Chadema.

Kwa sasa Profesa Lipumba amefikisha miongo miwili na nusu (miaka 25) katika wadhifa wa uenyekiti wa CUF.

Jina la Profesa Lipumba linachomoza katika kipindi ambacho kuliibuka uvumi hana mpango wa kutetea nafasi hiyo.

Hata hivyo, baadaye ikaelezwa mwanasiasa huyo mkongwe aliyewahi kuwania urais wa Tanzania kwa awamu nne mfululizo bila mafanikio, alichukuliwa fomu na wafuasi wake. Taarifa za kurejeshwa au kutorejeshwa fomu hiyo hazikuwekwa wazi.

Mwananchi lina taarifa za uhakika kuwa, Profesa Lipumba ni mmoja kati ya wagombea tisa wanaowania nafasi hiyo kwenye uchaguzi huo.

“Mwanzo kulikuwa na taarifa kwamba Profesa Lipumba hatagombea na alishaeleza hilo kwenye kikao cha kamati ya utendaji, lakini tunashangaa jina bado lipo,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF (jina limehifadhiwa).

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa amethibitisha kuwepo jina la Profesa Lipumba kama mmoja wa wagombea wa uenyekiti taifa.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari, kimeieleza Mwananchi kuwa majina ya wagombea wa nafasi hiyo yalipitishwa Desemba 15, 2024 na Baraza Kuu la Uongozi la CUF.

Orodha ya majina hayo kwa mujibu wa chanzo hicho, ilisomwa na Profesa Lipumba likiwamo jina lake.

Katika uchaguzi huo watakaochuana na Profesa Lipumba ni Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud ambaye alichukua wadhifa huo baada ya hayati Maalim Seif Shariff Hamad kujiondoa na kujiunga na ACT-Wazalendo.

Maalim Seif na kundi lake walijiengua CUF baada ya mgogoro kati yake na Profesa Lipumba uliodumu kwa miaka kadhaa.

Kama ilivyo kwa Mbowe, endapo atajitosa kuwania nafasi hiyo atachuana na makamu wake Bara, Tundu Lissu, Profesa Lipumba naye atachuana na makamu mwenyekiti (Bara), Maftah Nachuma.

Wengine ni Ali Hamisi, Athumani Kanali, Juma Nkumbi, Nkunyuntila Chiwale, Wilfred Rwakatare (Mbunge wa zamani wa Bukoba Mjini) na Chifu Yemba (aliyewahi kuwania urais kwa tiketi ya ADC 2020). Tayari majina yamepitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF na Ngulangwa amethibitisha wote wamo.

Kutokana na taarifa za uwepo wa Profesa Lipumba katika kinyang’anyiro hicho, Rwakatare aliyepitishwa kuwania nafasi hiyo ameahidi kujitoa iwapo atathibitisha kuwa mwenyekiti wake wa sasa ni miongoni mwa washindani wake.

“Msimamo wangu ni kwamba kama Profesa Lipumba anagombea, mimi sigombei sababu namheshimu. Wakati anakuwa mwenyekiti hakutaka kugombea mimi nilimshawishi sana.

“Kabla sijajaza fomu nilimuuliza mara tatu akaniambia hagombei na nikamwambia kama hugombei hiyo inanisukuma nichukue fomu, lakini kama unagombea siwezi kugombea naye,” amesema.

Tofauti na miaka ya nyuma ambako CUF ilikuwa na wanachama, viongozi na wafuasi wenye ushawishi mkubwa hata kwenye mikutano yake, uchaguzi unaofanyika Desemba 18 unaonekana kupoa na kukosa mvuto.

Mpaka sasa zikiwa zimesalia saa kadhaa kabla ya mkutano wa uchaguzi, hakuna harakati wala hamasa hivyo kuzidisha sintofahamu kuhusu mustakabali wa chama hicho kilichowahi kutikisa vilivyo siasa za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Kiama Mwaimu amesema hakuna shaka kwamba, Profesa Lipumba ni mwanasiasa mkongwe lakini, kukaa kwake madarakani kwa muda mrefu kunapoteza mvuto.

Amesema mwanasiasa huyo amedumu kwa miaka 25, hivyo uchaguzi unaweza kupoteza mvuto na ushawishi.

“Wanafanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba lakini hautakuwa na mvuto wala afya kama chaguzi nyingine. Si uchaguzi utakaoleta mwamko na hamasa kama ilivyokuwa kwa Chadema hivi sasa,” amesema.

Hali ya CUF bungeni, halmashauri

Tofauti na miaka 10 iliyopita ambayo CUF ilikuwa na idadi kubwa ya wawakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwenye Baraza la Wawakilishi, Zanzibar pamoja na madiwani kwenye halmashauri mbalimbali, kwa sasa hali yake ni mbaya. Katika uchaguzi wa mwaka 2015, CUF ilipata viti 32 vya ubunge wa majimbo.

Majimbo hayo ni Kilwa Kusini (Selemani Bungara), Tumbe (Rashid Ali Abdallah), Kiwani (Abdallah Haji Ali), Wete (Mbarouk Salim Ali) na Mchinga (Hamidu Bomali).

Mengine ni Gando (Othaman Haji), Konde (Khatib Said Haji), Wingwi (Juma Kombo Hamad), Chambani (Yussuph Salim Hussein), Mtambwe (Khalifa Mohamed Issa) na Micheweni (Haji Khatib Kai).

Lipo pia jimbo la Tandahimba (Katani Katani), Mwanakwerekwe (Ali Salim Khamis), Nungwi (Yussuph Haji Khamis), Chonga (Mohammed Juma Khatib) na Liwale (Zuberi Kuchauka).

Pia, Kojani (Hamad Salim Maalim), Chake Chake (Yussuph Kaiza Makame), Tanga Mjini (Mussa Mbarouk), Mkoani (Twahir Awesu Mohammed), Temeke (Abdallah Mtolea) na Kinondoni (Maulid Mtulia).

Mengine ni Bumbwini (Mohammed Mohammed), Kilwa Kaskazini (Vedastor Ngomalemwiru), Mtwara Mjini (Maftaha Nachuma), Wawi (Ahmed Juma Ngwali), Ole (Juma Hamad Omar), Ziwani (Nassor Suleiman Omar), Kaliua (Magdalena Sakaya), Malindi (Ally Abdulla Saleh), Mtambile (Masoud Abdallah Salim) na Mgogoni (Ally Yusuph Suleiman).

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, CUF ilipata viti vitatu vya ubunge wa majimbo, huku ikiambulia patupu kwa upande wa viti maalumu.

Majimbo ambayo chama hicho kilishinda ni Mtwara Vijijini (Shamsia Mtamba), Pandani (Maryam Said) na Mtambile (Seif Salum Seif).

Related Posts