RAIS MWINYI:NIMERIDHIKA NA KAZI YA ZPDB

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuridhishwa kwa utoaji na usimamizi wa vipaumbele vyote kwa sekta za umma hasa kwa miradi ya kimkakati.

Amesema, usimamizi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazotolewa na kuhakikisha utoaji huduma bora katika maeneo yote ya vipaumbele zikiwemo Elimu, Miundombinu, Uwezeshaji sekta ya Utalii na barabara.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 16 Disemba 2024 Ikulu Zanzibar, kwenye maadhimisho ya miaka miwili ya Taasisi ya Ofisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa utendaji Serikalini (ZPDB)

Aidha Rais Dk.Mwinyi amesema upatikanaji wa huduma za jamii kwa wakati ni Msingi wa Maendeleo na kigezo muhimu cha utawala bora na uongozi wenye kujali wananchi wake.

Kwa upande mwingine Rais Dk. Mwinyi amezitaka taasisi zote za Serikali kutoa ushirikiano wa kiutendaji kwa maofisa wa taasisi ya ZPDB kwani taasisi hiyo ipo chini yake na kutekeleza juhudu zake za maendeleo.

Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi ameonya kutotoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ni makosa na ameziagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua Watendaji na watumishi hao bila ya kumuonea mtu.

Rais Dk. Mwinyi pia ameeleza mafanikio ya ZPDB hayatapatikana bila ya ushirkiano wa kutosha kutoka taasisi nyengine za Serikali hivyo, amezitaka taasisi za umma kwa nafasi zao wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha nchi inazidi kupiga hatua za haraka za maendeleo katika kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii.


 

Related Posts