Dar es Salaam. Serikali imetangaza wanafunzi wote 974,332 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza baadaye mwakani, huku ikibainisha kwamba wataanza masomo bila kusubiri machaguo kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita.
Imesema kuwa kati ya wanafunzi hao wasichana ni 525,225 na wavulana ni 449,107 ambao wamechaguliwa kujiunga na shule za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu, Desemba 16, 2024, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, amesema hakutakuwa na utaratibu wa wanafunzi kujiunga na masomo kwa machaguo.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kwamba, Serikali ilifanya maandalizi ya kutosha mapema kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya shule zake ikiwemo vyumba vya madarasa. Katika miaka ya nyuma elimu ya Tanzania ilipita kwenye mtikisiko kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati ambapo, wanafunzi walilazimika kuchaguliwa kuanza kidato cha kwanza kwa machaguo.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kumekuwepo na kasi kubwa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na uboreshaji wa miundombinu katika shule za umma hivyo, changamoto ya uhaba wa madarasa kutosikika.
Kwa mujibu wa Mchengerwa kati ya wanafunzi hao waliofaulu, 809 wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari maalumu ambazo zinapokea ufaulu wa alama za juu zaidi.
Mbali na hao, Mchengerwa amesema wanafunzi wengine 1,174 wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za mkondo wa amali.
“Jumla ya wanafunzi 6,810 wakiwemo wasichana 5,199 na wavulana 1,611 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni za Serikali. Kati ya wanafunzi hao, wasichana 3,320 wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za wasichana za sayansi,” amesema.
Kwa upande wa shule za sekondari za kutwa, wanafunzi 965,539 wamechaguliwa kujiunga.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, mwaka 2025 hakutakuwa na utaratibu wa kusubiri machaguo kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza masomo, kwa kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya miundombinu yote.
Kutokana na hilo, amesema wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa shule za kutwa, watatakiwa kuripoti shuleni kuanzia Januari 13, 2025, huku wa bweni wakitakiwa Januari 12, 2025 tayari kwa kuanza masomo.
“Serikali ilifanya maandalizi mapema ili kuhakikisha wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2024 wanajiunga na elimu ya sekondari ifikapo Januari, 2025 bila vikwazo,” amesema.
Kwa kuwa utekelezaji wa mtalaa mpya ulishaanza, ameeleza kila shule ya sekondari itumie vema kipindi wanapoanza kupokea wanafunzi ili kuwajengea uwezo wa kuwasiliana katika lugha ya Kiingereza.
Pia, ametaka kipindi hicho kitumike kuchagua aina ya fani ambazo wanafunzi wanazopenda kusoma katika shule zenye mkondo wa amali zisizo za kihandisi.
Amewataka wazazi na walezi kufanya maandalizi ya kutosha kwa watoto waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza ili kuepuka kuchelewa kuanza masomo.
Amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri zote kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na sekondari wanaripoti shuleni na kuandikishwa.
“Ninawaagiza wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa shule kuhakikisha maandalizi yote kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi yanakamilika,” amesema.