Serikali yaja na sharti jipya ‘plea bargaining’

Dar es Salaam. Serikali imeweka sharti jipya la mshtakiwa wa kesi ya jinai au uhujumu uchumi, kumaliza kesi kwa utaratibu wa majadiliano na makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP),  ambapoo mshtakiwa atalazimika kusubiri mpaka upelelezi wa kesi ukamilike.

Sharti hilo limetajwa na mwendesha mashtaka kwenye kesi dhidi ya Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi iliyotajwa leo Desemba 16, 2024. Gasaya anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 8/2024, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili; la kujipatia Sh5.1 bilioni na la pili la utakatishaji fedha.

Anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (Saccos) cha kampuni ya Jatu, kwa madai ya kwenda kuzipanda katika kilimo cha mazao ili kupata faida zaidi kwa wanachama.

Kutokana na kesi hiyo,  Gasaya ambaye amekaa mahabusu tangu aliposomewa mashtaka mwaka jana kwa kuwa shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana, aliomba kufanya majadiliano na DPP ili kufikia makubaliano ya kumaliza kesi kwa utaratibu wa ‘Plea bargaining’.

Wakati kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhina ilipotajwa leo, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Frank Romuli ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika akaomba ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Denis Mniko kwa niaba ya Wakili Nafikike Mwamboma anayemtetea Gasaya, ameomba upande wa mashtaka, ujitahidi kukamilisha upelelezi ili kesi iendelee katika hatua inayofuata akidai mshtakiwa amekaa gerezani muda mrefu.

Gasaya aliomba nafasi ya kuzungumza, aliporuhusiwa pamoja na mambo mengine amehoji hatima ya mchakato wa plea bargaining yake.

“Shauri hili lilishafikia mchakato wa plea bargaining na walalamikaji ambao ndio hawa hapa walishakubali  kuwa tukishakubaliana linakuwa limeisha lakini baada ya hapo hakuna kinachoendelea, naomba  utoe maelekezo,” amesema Gasaya.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Rumoli amesema utaratibu wa plea bargaining kwa sasa umebadilka.

“Hivi sasa kuna maelekezo kuwa plea bargaining isifanyike mpaka upelelezi umekamilika ndiyo maana unasuasua, lakini bado mchakato upo,” amesema.

Gasaya amesema kwa kuwa  nafasi ya majadiliano na makubaliano hayo bado ipo, ameomba waendelee akidai DPP alishaonana naye na kuzungumza kuhusu hilo, lakini akaomba mahakama iuelekeze upande wa mashtaka kwa tarehe ijayo upeleke majibu ya hatima ya upelelezi wa kesi yake.

“Naomba Mahakama yako imuelekeze Wakili wa Serikali na kikao kijacho aje na majibu sahihi ya upelelezi ulikofikia,” amesema.

Hakimu Mhina amekubali ombi la Gasaya akautaka upande wa mashtaka kueleza uhalisia wa maendeleo ya upelelezi.

“Safari ijayo tunataka kupata position (hali) halisi kuhusu upelelezi lakini na plea kama inawezekana. Naahirisha kesi hii mpaka Desemba 30, 2024,” amesema.

Katika shtaka la kwanza, Gasaya anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.1 bilioni kutoka Saccos ya JATU.

Anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya JATU kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua si kweli

Shtaka la pili anadaiwa siku na eneo hilohilo akiwa mtendaji mkuu na mwanzilishi wa JATU Saccos, alitakatisha Sh5.1 bilioni.

Anadaiwa siku hiyo alijihusisha na muamala wa kiasi hicho cha fedha kutoka akaunti ya JATU Saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda akaunti ya JATU PLC liyopo benki ya NMB tawi la Temeke.

Anadaiwa alitenda kosa hilo wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Related Posts