Singida BS yaiacha hoi Prisons ikizishusha Simba na Yanga

Mabao mawili ya Marouf Tchakei dakika ya 47 na Kennedy Juma dakika ya 58, yametosha kuipa pointi tatu Singida Black Stars ikiizima Tanzania Prisons na kuchumpa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikizishusha Simba na Yanga.

Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo kuvuna pointi sita kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa baada ya awali kuifumua KenGold mabao 1-3 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara.

Ushindi huo unaifanya Singida Black Stars kuendeleza ubabe kwa Maafande hao kwani katika michezo sita waliyokutana tangu ilipokuwa ikiitwa Ihefu wameshinda minne, sare moja na kupoteza mmoja.

Wakati Singida Black Stars ikipanda nafasi ya pili kwa pointi 30 sawa na vinara Azam FC, zikitofautiana wastani wa mabao, Prisons wanabaki nafasi ya 14 kwa pointi 11 baada ya michezo 14 kila timu.

Katika mchezo wa leo uliopigwa saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Sokoine, ilishuhudiwa dakika 45 za kwanza timu zote zikienda mapumziko bila bao kabla ya kipindi cha pili kuwanyookea Singida Black Stars kwa ushindi huo.

Kaimu Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Ramadhan Nsanzurwimo amesema baada ya wapinzani kuingia kwa uhitaji wa sare, waliamua kuwafungua na kufanikiwa kupenya na kupata ushindi huo.

Amesema Prisons anaifahamu vyema tangu alipokutana nayo akiwa Mbeya City, hivyo aliiona kama ‘Dabi’ akihitaji kupata pointi tatu jambo ambalo amefanikiwa.

“Kwa ujumla haukuwa mchezo rahisi, Prisons waliingia kucheza kujilinda na kucheza rafu nyingi ambazo hazikuwa na sababu, tukaamua kipindi cha pili kuwafungua na wakaingia mtegoni tukaondoka na ushindi,” amesema Nsanzurwimo.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Prisons, Mbwana Makata amesema pamoja na matokeo magumu, wanaenda kurekebisha makosa haswa dirisha dogo kwa kuongeza nguvu katika maeneo ya ushambuliaji na kiungo.

“Tutafanyia kazi maeneo yenye upungufu kwa kuongeza nguvu eneo la straika na kiungo, naamini raundi ya pili itakuwa na mabadiliko mazuri tutaondoka nafasi za chini,” amesema Makata.

Related Posts