Ushauri kwa wizara upelekaji fedha kwa halmashauri

Dodoma. Wizara za kisekta zimeshauriwa kuhakikisha zinapeleka fedha kutekeleza vipaumbele vyao kwenye halmashauri kuwezesha miradi kutekelezwa bila vikwazo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Leo Mavika amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 16, 2024 alipotoa mada kwenye mkutano wa wadau wa serikali za mitaa ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi Institute.

Mavika aliyewahi kuwa mkurugenzi wa halmashauri, amesema wizara nyingi hazipeleki fedha kwenye halmashauri, hali inayosababisha miradi kuonekana kama ni ya Serikali Kuu.

“Fedha za miradi ya kipaumbele za wizara za kisekta zinapaswa kuelekezwa moja kwa moja kwenye halmashauri, ili miradi hiyo iweze kutekelezwa ipasavyo,” amesema.

Ametoa mfano wa mradi mmoja wa kipaumbele wa wizara ambao haukupewa fedha, badala yake halmashauri husika ilitenga bajeti isiyozidi Sh700,000.

Kauli hiyo ilipokewa kwa makofi kutoka kwa baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri waliohudhuria mkutano huo. Wakurugenzi 52 kati ya 184 walihudhuria.

Amesema kuna haja ya kuboresha uratibu kati ya miradi ya kipaumbele ya wizara za kisekta na ya halmashauri, ili kuondoa mgongano unaojitokeza.

Mavika amebainisha kuwa mkurugenzi wa halmashauri ndiye ‘katibu mkuu’ wa kila wizara, kwani wizara zote zinapofanya kazi kwenye halmashauri hushirikiana na mkurugenzi.

Amesisitiza umuhimu wa wakurugenzi kupewa washauri wenye ujuzi wa kutosha, badala ya kuwaajiri wahitimu wa vyuo vikuu moja kwa moja kwenye nafasi zinazowapa fursa ya kuwa washauri wa wakurugenzi.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Institute, Kadari Singo, amesema takriban asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika katika serikali za mitaa kuhudumia wananchi.

“Hivyo, kuanzisha mradi bila kushirikisha wananchi kujua wanataka nini ni changamoto kubwa,” amesema.

Ametoa mfano wa mji mmoja ambao Serikali ilijenga maktaba bila kushirikisha wananchi, matokeo yake maktaba hiyo ilitumiwa zaidi kama kituo cha kulea watoto badala ya kuwa mahali pa kujisomea.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Dk Festo Dugange, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kushughulikia changamoto za maendeleo kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu.

“Kuna halmashauri ambazo zilikuwa na changamoto nyingi, lakini tulipobadilisha mkurugenzi, matatizo yalianza kupungua,” amesema.

Dk Dugange amewahimiza wakurugenzi kujadili changamoto za kisera, kisheria na kitaasisi wanazokumbana nazo na kutoa mapendekezo ya kuzitatua.

Pia, ameonya kuhusu miradi kutokamilika kwa wakati na kwa gharama zilizopangwa.

“Fedha za mradi zimetengwa Sh600 milioni lakini ujenzi unafika asilimia 40 na fedha zinaisha. Kisha mnaomba nyongeza ya Sh300 milioni. Hii haiwezekani,” amesema.

Related Posts