Utata mwili wa Ulomi ukipatikana Mwananyamala

Dar es Salaam. Siku tano tangu mfanyabiashara Daisle Ulomi alipopotea Desemba 11, 2024,  mwili wake umekutwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam leo Desemba 16.

Ulomi aliyekuwa akifanya biashara za fedha za mitandao ya simu maeneo ya Sinza Kijiweni na Mwenge, jijini Dar es Salaam, alipotea katika mazingira yenye utata.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro katika taarifa aliyoitoa leo jioni amesema: “Ufuatiliaji umefanyika kwa kushirikiana na ndugu na kubainika kuwa Ulomi alipelekwa Kituo cha Afya cha Makuburi, Ubungo External mchana wa Desemba 11, 2024 baada ya kupata ajali mbaya na pikipiki aliyokuwa akiitumia.

“Wasamaria wema walimsaidia kumpeleka kwenye Kituo cha Afya cha Makuburi, External Ubungo akiwa hajitambui na hakuwa na kitambulisho chochote. Baadaye alipelekwa Mwananyamala hospitali na ikabainika tayari alikuwa amefariki.”

Kamanda Muliro amesema mwili ulihifadhiwa hospitalini hapo kama mtu asiyefahamika akisubiri kutambuliwa na ndugu.

“Ndugu tayari wameutambua mwili huo ukiwa na majeraha maeneo mbalimbali ya mwili. Aidha, pikipiki aliyopata nayo ajali pia imepatikana ikiwa imeharibika. Uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea na taarifa zaidi itatolewa,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Japhet Munisi aliyejitambulisha kuwa ni mkwe wa Ulomi alisema alipigiwa simu leo asubuhi na mke wa marehemu, akimjulisha kuwa alipata taarifa kuwa mwili wa mumewe uko hospitali.

“Baada ya kupata taarifa nilifika Hospitali ya Mwananyamala na kukuta askari wakiwa eneo la kuhifadhia maiti. Niliwauliza wahudumu pale hawakutaka kunieleza lolote.

“Niliwauliza askari waliokuwepo eneo hilo nao wakasema wanafanya uchunguzi kwanza ndipo watatoa taarifa,” amesema Munisi.

Amesema ndugu wanakusanyika Mikocheni nyumbani kwa Ulomi kupanga taratibu za mazishi, huku wakisubiri taarifa ya Polisi.

Nyumbani hapo wamefika waombolezaji ambao wamekuwa wakikaa kwa vikundi wakionekana kujadiliana.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwananyamala, Dk Zaver Benela alipotafutwa na Mwananchi, amesema mwili wa Ulomi ulifikishwa hospitalini hapo Desemba 11, 2024 ukitokea Wilaya ya Ubungo.

“Mwili wa Ulomi ulifikishwa hapa siku hiyo mchana na maelezo yaliyopo hapa alitokea Zahanati ya Makuburi sasa hapo la zaidi ni kuwatafuta polisi na hicho kituo wanaweza kuwa na maelezo zaidi,” amesema.

Amesema kwa kuwa tukio lilitokea mchana majeraha aliyokutwa nayo ni kama mtu aliyepata ajali, hivyo maelezo zaidi yanaweza kupatika eneo alilotaja.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makuburi, Alphoncina Mbinda amesema walimpokea majeruhi aliyepelekwa hospitalini hapo na Jeshi la Polisi lakini hakufahamika jina.

“Majeruhi aliletwa na askari wakisema alipata ajali iliyohusisha lori na pikipiki. Majeruhi hakuwa na uwezo wa kuzungumza, hivyo tukaita gari la wagonjwa haraka na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala,” amesema

Taarifa nyingine iliyosambaa mtandaoni ilimkariri Katibu wa hospitali ya Mwananyamala, Lydia Nzema akisema walipokea mwili wa mfanyabiashata huyo Desemba 11, 2024 ukitokea Zahanati ya Makuburi ikielezwa kifo chake kimetokana na ajali.

“Hii ikiwa na maana kama ni kituo cha afya alichopelekwa kwa ajili ya matibabu ilikuwa ni Zahanati ya Makuburi na sisi tumepokea kutoka zahanati hiyo mwili ambao haujatambuliwa na tulihifadhi katika chumba cha maiti kama ilivyo kwa miili mingine,” amesema na kwamba ulitambuliwa Desemba 16.

Desemba 15, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilieleza kuanza kumtafuta Ulomi aliyetoweka katika mazingira yenye utata, Desemba 11 akiwa kazini kwake Sinza Kijiweni.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa juzi, Ulomi hakurudi nyumbani tangu alipoingia kazini kwake, ikidaiwa siku hiyo alionekana akitoka ofisini Sinza Kijiweni saa sita mchana kuelekea Mbagala, Bandari Kavu.

Katika taarifa hiyo, kamanda Muliro alisema wakati mfanyabiashara huyo anaondoka inadaiwa alikuwa anakwenda kukagua kontena la bidhaa zake baada ya kuitwa na watu waliodai walikuwa wanashughulikia kulitoa bandarini.

“Jeshi linaendelea na ufuatiliaji wa taarifa hiyo kwa kushirikiana na ndugu ili kujua na kubaini yupo wapi,” ilieleza taarifa.

Kamanda Muliro alisema Desemba 12, katika kituo cha Polisi Chang’ombe ilipokewa taarifa ya kutafutwa  mfanyabiashara huyo kutoka kwa familia yake.

“Taarifa hiyo inadai Ulomi alikuwa anatumia usafiri wa pikipiki namba MC 415 DQC aliyokuwa akiendesha mwenyewe. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusiana na mtu huyo azitoe kwenye mamlaka yoyote ya Serikali iliyo karibu yake,” ilisema taarifa ya Polisi.

Elizabeth Munisi, mkewe Ulomi juzi alilieleza Mwananchi kuwa tangu alipotoa taarifa Polisi kuhusu kupotelewa na mume Desemba 12, alikuwa njia panda kwani hawakujua aliko.

“Jana (Desemba 14) asubuhi nilipigiwa simu na RPC wa Temeke kuniambia bado hawajamuona na wanaendelea kumtafuta, lakini kwa leo bado hawajanipa mrejesho wowote, nasubiri,” alisema.

Awali, kupitia mitandao ya kijamii kulisambaa taarifa ikieleza mfanyabiashara huyo alipotea wakati anaelekea bandari kavu alikoitwa na watu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kupitia mtandao wa X,  Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob aliandika akidai mfanyabiashara huyo alikwenda bandari kavu kukagua kontena lake baada ya kuitwa na watu wa TRA kwa ajili ya ukaguzi.

Desemba 14, TRA kupitia kitengo cha Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano ilitoa taarifa kujitenga na tukio la kupotea Ulomi.

“TRA inautaarifu umma kuwa, mchakato wa uondoshaji wa mizigo bandarini hufanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu za kiforodha. Kwa mujibu wa kifungu cha 2(1) cha Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki, ni wakala wa forodha peke yake ndiye anayewajibika kusimamia taratibu zote za kiforodha za uondoshaji wa mizigo bandarini kwa niaba ya mwagizaji wa mzigo na siyo mwagizaji wa mzigo.

“Kwa mujibu wa kumbukumbu zetu, mfanyabiashara, Daisle Simon Ulomi aliichagua kampuni ya wakala wa forodha ya Twende Freight Forwarders Limited kupitia barua yake kwa TRA ya Desemba 5, 2024 kuwajibika kuondosha mizigo yake bandarini kulingana na taratibu za forodha,” ilieleza taarifa hiyo.

TRA ilisema imekuwa ikifanya kazi na wakala wake ambaye bado hajakamilisha taratibu za kiforodha kuondosha mzigo husika na kwamba, TRA haijawahi kumuita wala kufanya naye kazi mfanyabiashara huyo katika ofisi zake kwa jambo lolote.

“Suala la kutoonekana kwa mfanyabiashara huyo ni jambo la kipolisi ambalo TRA haihusiki nalo,” ilisema taarifa hiyo.

Related Posts