Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wakazi wa Kawe wakitumia fursa ya uwepo wa Kanisa la Inuka Uangaze la Nabii na Mtume Boniface Mwamposa, imebainika wapo waumini wanaotoka mikoani wakikabiliwa na adha ya malazi, kukosa faragha na kuhatarisha afya zao.
Mwananchi katika uchunguzi wake, imebaini mitaa ya Ukwamani na Mzimuni kuna nyumba zinazolaza waumini hao, kwa wastani moja inalaza hadi watu 60, wakubwa kwa wadogo wakiwamo watoto wa umri chini ya miaka mitano.
Kutokana na idadi kubwa ya watu, vyoo vilivyopo havitoshelezi mahitaji, hivyo kuhatarisha afya za watumiaji wake.
Malipo ya malazi hutozwa kulingana na aina ya nyumba na vyumba ikianzia Sh1,000 hadi Sh6,000 kwa usiku mmoja. Mbali ya wanaolala ndani, wapo pia wanaokaa nje.
Kwa anayehitaji shuka hukodi kwa Sh1,000, huku anayehitaji kuoga hulipia Sh500.
Licha ya baadhi kuibiwa hasa simu, wakati mwingine ndani ya vyumba au nyumba unaweza usipate usingizi kutokana na watu wanaosumbuliwa na pepo. Kwa mujibu wa mzee Salum Silanga (si jina halisi), mkazi wa Kawe, waumini wanaolala wanafanya hivyo ili kuwahi viti vya mbele wakati wa ibada ya kwanza Jumapili inayoanza saa moja asubuhi. Anasema waumini huanza kufika kanisani hapo saa nane usiku.
Akizungumzia mtaa wa Mzimuni, anasema ni kama vile kusema mgeni aje mwenyeji apone, kwani wenye nyumba wameacha kupangisha kwa mwezi badala yake huzitumia kulaza waumini.
“Fursa hii imekuja baada ya Mwamposa kuweka walinzi kanisani kuzuia watu kulala eneo hil, hivyo walianza kuja kulala huku na wanalipa kwa siku,” amesema.
Anasema katika nyumba moja hulala watu wengi, huku wamiliki wakiwapatia mikeka.
Wakati hayo yakifanyika, Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999, kifungu cha 79 kinaeleza haki, wajibu na taratibu za upangishaji wa ardhi, nyumba na sehemu za malazi.
Kifungu hicho kinasisitiza mkataba wa upangishaji unapaswa kuwa wa maandishi na kuainisha masharti ya upangishaji. Ni dhahiri kwamba kinachofanyika kinakiuka sheria.
Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule mwishoni mwa Novemba, 2024 aliahidi kufuatilia jambo hilo, kulifanyia kazi na kulichukulia hatua.
“Nyumba za kulala wageni zina utaratibu wake, si kila nyumba inaruhusiwa kulaza wageni, tunafahamu wakati mwingine matendo ya kikatili yanafanyika nyumbani kwa kuwakaribisha watu usiowajua,” amesema.
Amesema kupokea watu wasiojulikana ni hatari kwa usalama wao, kwani kuna uwezekano wa kupokea watu wengine wenye tabia za kihalifu.
“Tutapita hapo pamoja na viongozi wa mtaa, kata na Jeshi la Polisi hasa mitaa ya Ukwamani na Mzimuni tutaongea na wananchi ili kuzidisha mahusiano na kanisa, lakini mitaa wanayoishi pia ili adui akija asiingie ndani hadi wajiridhishe,” amesema.
Mtambule amesema walishakaa na Mwamposa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo.
“Tulikubaliana ratiba za ibada ziwekwe vizuri ili waumini waweze kuhudhuria na kupata muda wa kuondoka kwa hiyo tumeimarisha ulinzi na usalama kwa wanaokwenda kuabudu pale,” amesema.
Mwanachi limemtafuta Mwamposa bila mafanikio kuzungumzia hilo. Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa kanisa hilo aliyeomba kutotajwa jina kwa kuwa si msemaji amesema baada ya kikao na Serikali walianza utekelezaji kwa kukataza watu kulala maeneo ya viwanja na ndani ya kanisa kwa ajili ya usalama wao.
“Kwa sasa tumeweka walinzi wanazunguka kuhakikisha watu hawalali maeneo ya kanisa kwa ajili ya usalama wao baada ya kutokea matukio kadhaa, yakiwemo ya uporaji na ubakaji lakini bado kuna watu hawakubali,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amesema wapo wananchi wanaokaa maeneo ya jirani wameamua kuwapangisha waumini wanaofika katika ibada ili kuwaweka katika usalama.
“Si kila anayepita humu ni mzuri wengine ni waovu na hatuwajui kwa kuwatazama, kwani watu hawajuani hilo tunawasisitizia kila wanapofika kanisani,” amesema.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini unapofika kwenye nyumba unakaribishwa na msimamizi anayepokea wageni, anakuuliza jina na kukutajia gharama za malazi.
“Kulala nje ni Sh1,000 na ndani Sh2,000 kwa hiyo ni uamuzi wako, ukishachagua unalipa halafu unaangalia sehemu yenye nafasi unaweza kulala hapo hata kwenye benchi ruksa,” anasema msimamizi katika nyumba moja.
Ukishachagua pa kulala unalazimika kulipia kwanza. Kwa wanaolala nje wanachanganyika wanawake na wanaume ambao hutumia mikeka.
“Kama kuna mtu anahitaji kuhifadhiwa simu alete maana kila mmoja ana shida zake usimuamini uliyelala naye, kama unaweza kuitunza basi baki nayo,” ni matangazo yanayotolewa na wasimamizi wa nyumba.
Kutokana na wingi wa watu wanaokuwapo kwenye nyumba, huduma ya choo ni kwa kusubiriana, baadhi wakijisaidia kwenye vichochoro. Katika baadhi ya nyumba hutumika vyoo vya shimo.
“Ni ngumu tunapokuwa wengi, hali ya vyoo na bafu inakuwa mbaya. Kuna wakati tunatumia vyoo kwa zamu, jambo linalosababisha kero kubwa,” anasema Mwanaidi Hamisi, aliyefika kuhudhuria ibada akitokea mkoani Tanga.
Anasema katika nyumba aliyolala kuna ndoo ya maji na kila mwanamke aliyelala hapo alitakiwa kuwa na chupa ambayo aliitumia kuchota maji na kwenda nayo msalani.
“Humu ndani choo ni kimoja na tunaolala nje ni wengi foleni imenifanya nitoke nje, tofauti na wanaolala ndani wapo wachache foleni yao haiwi kubwa kama yetu,” anasema.
Mathias Moga kutoka mkoani Iringa, amesema ana mwezi mmoja tangu alipofika kanisani hapo ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazomkabili.
“Nimemaliza chuo tangu mwaka 2014 fani ya ualimu, wadogo zangu wote wamepata ajira na kaka zangu kasoro mimi, kusema kweli najisikia vibaya nimebaki kama mkiwa,” amesema Moga.
Silvelius Mwaluka, mkazi wa mkoani Katavi amesema ana mwezi mmoja tangu alipofika kanisani hapo kuiombea familia yake inayosumbuliwa na maradhi.
Amesema wengi wanaolala katika maeneo hayo wanakabiliwa na matatizo ya kifamilia, ikiwepo mifarakano ya mke na mume, madeni, maradhi yasioisha na kukosa ajira.
“Nikisikia tangazo la ibada ya kufunguliwa nakuja bila kuwaza, nipo tayari kutumia gharama kwa ajili hiyo tu. Kama sasa hivi nina madeni sijui pesa nimefanyia nini na nimefarakana na watoto wangu sijui natatua vipi changamoto hizi,” anaeleza mama ambaye hakuwa tayari kutajwa jina.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameeleza wasiwasi wao kuhusu kupokea wageni wasiowafahamu.
“Hatuwajui hawa watu wanaokuja kulala hapa kwa siku moja ni vigumu kujua kama kweli wamekuja kwa nia njema au wana mambo mengine,” amesema Omary Seif, mkazi wa eneo la Maringo.
Amesema licha ya kuwapo fursa za kiuchumi, hali hiyo inahitaji uangalizi mkubwa ili kudhibiti masuala ya uhalifu.
Anastazia Maganga (45), mwenye nyumba eneo la Masae amesema mahitaji ya malazi wakati wa ibada ya Jumapili, Jumatatu na kipindi cha matukio makubwa imekuwa fursa kwake kwa kuwa ana uhakika wa kuingiza fedha.
“Huwa napokea watu wengi tu wakati wa ibada za Nabii. Wengine wanakuwa na uwezo wa kulipia kitanda, kwenye mikeka na magodoro. Kwa siku kama mbili hivi ninaweza kupata zaidi ya Sh100,000,” amesema.
Amesema wanaolipa Sh1,000 wanalala kwenye mikeka nje, Sh2,000 wanalala sebuleni na chumbani, huku wanaolipa Sh5,000 wanalala kwenye magodoro na kitandani.
Anastanzia anasema wanakodisha mashuka kwa wahitaji na hasa wanaume hulipia Sh1,000.
Salumu Hamduni ambaye nyumba yake ina vyumba vitatu na uwanja mkubwa, amesema idadi ya wageni huwa kubwa kiasi cha kumlazimu hata kuwashawishi majirani zake wakubali kuwapokea.
“Ni fursa nzuri kwetu, lakini changamoto pia kwa afya zetu maana watu tunaowakaribisha ni wengi na choo ni kimoja na hapa wapo wasafi na wachafu kila mmoja na tabia zake,” Amesema na kuongeza kuwa suala la kuhakikisha usafi linakuwa gumu kutokana na idadi kubwa ya watu.
“Najaribu kadri ya uwezo wangu kuweka usafi, lakini ukiwa na wageni zaidi ya 50 ni changamoto,” amesema.
Daktari katika hospitali iliyopo Wilaya ya Kinondoni, Rashid Hamisi, amesema kusongamana kwa watu kwenye nyumba moja kunakuwa na uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa ya kuambukiza kwa njia ya hewa, magonjwa ya tumbo na ngozi.
“Magonjwa ya mfumo wa hewa kama kikohozi yanaweza kusambaa haraka pale watu wengi wanapokaa eneo dogo pasipo uingizaji mzuri wa hewa. Hali kama hiyo pia inachangia kupungua kwa ubora wa usingizi wa wageni, jambo ambalo linaathiri afya zao,” amesema.
Amesema watoto wanakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya magonjwa ya njia ya hewa kutokana na uingizaji duni wa hewa katika maeneo yenye watu wengi.
“Wanapolazimika kulala karibu na watu wengi, wanaweza kupata maambukizi ya magonjwa ya ngozi na fangasi kwa sababu ya kugusa vitu au sakafu zenye usafi hafifu,” anasema.
Dk Rashid amependekeza umuhimu wa wenye nyumba kuwa na utaratibu maalumu wa usafi, ikiwemo kuhakikisha vyoo vinasafishwa mara kwa mara na kutoa maelekezo kwa wageni kuhusu masuala ya kiafya na usafi wa mwili.