VIONGOZI WA MABARAZA YA VIJANA WA SHEHIA KUPATIWA MAFUNZO AFYA YA UZAZI

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan amesema kupatiwa Vijana elimu ya afya ya uzazi na udhalilishaji kuna jenga uelewa juu ya kufahamu njia sahihi za kutatua changamoto zinazowakabili.

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunguwa mafunzo ya Afya ya Uzazi, Udhalilishaji pamoja na Sera ya Maendeleo ya Vijana kwa Viongozi wa Mabaraza ya Vijana ya Shehia za Unguja huko katika Ukumbi wa Kituo cha Mafunzo ya Vijana (YTC) Bweleo Wilaya ya Magharibi ‘B’.

Amesema Vijana wanapitia katika mazingira magumu ikiwemo kukutana na vishawishi hivyo elimu hiyo itawapa mbinu sahihi za kuweza kujikinga na mambo maovu yanayoweza kuwakumba.

Aidha Vijana ndio Taifa la kesho na kuwataka kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao katika kuhamasisha, kuelimisha na kushauri mambo mazuri yanayoendana na Maadili ya Nchi yao.

‘’ Mumechaguliwa nyinyi Viongozi katika Shehia zenu, ninawaomba muwe makini, munatakiwa kuwa mfano bora katika kupiga vita vitendo vinavyoashiria Udhalilishaji katika jamii’’alisema Katibu huyo.

Aidha amewataka Vijana ambao wapo mitaani bado hawajajiunga na Mabaraza hayo, kujiunga ili kupatiwa fursa mbali mbali zinazojitokeza ikiwemo kujengewa uwezo.

Nae Mkufunzi Farida Juma Haji amesema Serikali inachukuwa juhudi ya kuwapa taaluma sahihi Vijana ili waweze kujiepusha na vitendo vya udhalilishaji na kubaki salama.

Amesema dhamira ya Serikali kupitia Idara ya maendeleo ya Vijana ni kukuza ustawi wa maendeleo, kuwajengea mazingira rafiki, yatakayowawezesha Vijana kushiriki kikamilifu katika sekta ya kiuchumi, Kisiasa na kijamii.

Kwa upande wa Katibu wa Baraza la Vijana Shehia ya Bububu Aisha Juma Abdalla amefurahishwa na mafunzo hayo kwani yatawasaidia kujua namna ya kujiandaa na masuala ya afya ya uzazi.

Aidha ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kujenga vituo vya amali ili kuweza kuwapatia Vijana mafunzo, yatakayowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.

Mafunzo hayo ya siku tatu, yameandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kupitia Idara ya Vijana chini ya Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa,linaoshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA).

Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano.
 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan akizungumza na Viongozi wa Mabaraza ya Vijana ngazi ya Shehia na Wilaya za Unguja katika Ukumbi wa Kituo cha Mafunzo ya Vijana (YTC) Bweleo Wilaya ya Magharibi B.
 

Baadhi ya Viongozi wa Mabaraza ya Vijana wa Shehia na Wilaya za Unguja wakisikiliza maelezo kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan (hayupo pichani) katika mafunzo ya Afya ya Uzazi na Udhalilishaji huko Kituo cha Mafunzo ya Vijana (YTC) Bweleo Wilaya ya Magharibi ‘B’.
 

 Picha ya pamoja kati ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan, Viongozi wa Mabaraza ya Vijana ngazi ya Shehia na Wilaya za Unguja,pamoja na Viongozi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana katika kituo cha Mafunzo ya Vijana ( YTC) Bweleo Wilaya ya Magharibi ‘B’.

Related Posts