WANAFUNZI 21 wa shule ya Msingi Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam wamewasili kwenye mji wa Istambul Uturuki kwaajili ya ziara ya kimasomo na utalii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wanafunzi hao wakiambatana na baadhi ya walimu wa shule hiyo walisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kwenda nchini humo na watakuwa nchini humo kwa siku 10.
Mkuu wa msafara huo, Goodluck Karashani alisema jana kuwa wanafunzi hao ni wale walio kwenye chama cha skauti shuleni hapo na kwamba imekuwa utaratibu wa kawaida wanafunzi wa shule hiyo kutembelea nchi mbalimbali kwa lengo la kujifunza mambo mapya ya elimu na masuala ya skauti.
Alisema wanafunzi hao wanapofika kwenye nchi mbalimbali hujifunza mambo mapya ambayo yanawajenga kiakili na kuwajengea uwezo wa kujiamini kwenye shughuli mbalimbali wanazofanya.
“Umekuwa utaratibu wa kawaida kwa vijana wetu wa skauti kutembelea mataifa mbalimbali kujifunza tamaduni mbalimbali za mataifa mengine kwa hiyo ziara hii ya kielimu huwa tunaamini kwamba zinasaidia kuwajenga wanafunzi wetu kiakili,” alisema
Alisema kila mwaka kundi la wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakitembelea nchi mbalimbali kwa malengo kama hayo ya kuwajengea uwezo wanafunzi hao wa kujiamini na kuona mambo mapya kwingine duniani.
“Tusiime ni shule kubwa na mambo yake ni makubwa kama haya kupeleka wanafunzi nje ya nchi kwa ziara za mafunzo kila mwaka siyo jambo dogo, tunaupongeza uongozi wa shule ya Tusiime kwa kuweka kipaumbele masuala ya taaluma na kuwajengea wanafunzi hali ya kujiamini,” alisema
“Kuwapa wanafunzi fursa kama hizi ndiko kunaifanya shule ya Tusiime kuendelea kufanya vizuri kwenye mitihani yake ya kitaifa na hata Mkoa wa Dar es Salaam, ukiangalia matokeo ya Tusiime kila mwaka yako juu kwasababu ya mambo kama haya,” alisema.