ZIKIWA zimebaki siku tano kabla ya Klabu ya Coastal Union kufanya uchaguzi wa viongozi, Desemba 21 mwaka huu, leo Jumanne kampeni zinatarajiwa kuanza kushika kasi kwa wagombea kujinadi kwa wanachama kuomba kura.
Coastal inatarajiwa kufanya uchaguzi huo baada ya wagombea 17 kupitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo huku nafasi ya mwenyekiti ikionekana kutokuwa na presha kutokana na Hassan Ramadhani Muhsin kukosa mpinzani baada ya aliyekuwa akiwania naye kuenguliwa na katiba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Coastal Union, Emmanuel Kiariro, alisema mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa ratiba kuanzia leo ndiyo muda wa wagombea kuanza kunadi sera zao kabla ya Desemba 21 kufanyika zoezi lenyewe.
“Ratiba imeenda kama ilivyopangwa, leo (jana Jumatatu) tumebandika majina 17 yaliyopitishwa, hakuna mgombea aliyekata rufaa baada ya kuenguliwa na katiba, kuanzia kesho (leo Jumanne) ni wakati wa wagombea kujinadi,” alisema.
Wakati huohuo, Kiariro amewataja wagombea wa nafasi mbalimbali waliopitishwa huku nafasi ya mwenyekiti akibaki mmoja Hassan Ramadhan Muhsin, nafasi ya Makamu Mwenyekiti inagombewa na Dk. Fungo Ali Fungo na Mohammed Kiruasha Mohammed.
Kwa upande wa Wajumbe kuna Hussein Abdallah Moor, Khamis Seleh Khamis, Emmanuel Abdallah Mchechu, Saida Said Bawazir, Nassor Mohammed Nassor, Hafidh Nassor Suleiman, Abdallah Zubeir Unenge, Mohammed Maulid Rajab, Baraka Mohammed Baraka, Injinia Baraka Fumbwe, Ally Saleh Sechonge, Hussein Ally Mwinyihamis, Sudi Said Hilal na Wazir Mohammed Wazir.