Air France yarejesha huduma zake KIA baada ya miaka 28

Hai. Wakati idadi ya watalii wanaoingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ikiongezeka kutoka 900,000 hadi milioni moja, Shirika la Ndege la Ufaransa (Air France) limerejesha huduma zake katika uwanja huo baada ya kusitisha kwa miaka 28.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Desemba 17, 2024 na Mkurugenzi wa Uwanja wa KIA, Rehema Myeya wakati wa uzinduzi wa wiki ya huduma ya usalama wa usafiri wa anga katika viwanja hivyo.

Ndege ya shirika hilo linaloongoza kati ya mashirika makubwa ya ndege barani Ulaya, ilitua KIA kwa mara ya kwanza Novemba 20, 2024 na sasa ndege hiyo itakuwa ikitua mara tatu kwa wiki uwanjani hapo na kurejea Uwanja wa Charles de Gaulle, Ufaransa kwa kutumia ndege yake mpya aina ya Airbus A350-900WXB.

“Mwaka huu tumepokea ndege ya Air France, ambayo ilisitisha huduma zake tangu mwaka 1996, lakini imerejesha huduma zake hapa katika uwanja wetu wa KIA,” amesema Myeya.

Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya kuimarishwa kwa usalama wa anga katika uwanja huo.

Amesema na sasa sekta ya utalii ina mchango mkubwa wa mapato ya uwanja huo kwa kuwa  unapokea zaidi ya watalii milioni moja kila mwaka.

“Kilimanjaro tumefaidika sana na suala la utalii kwa sababu kiwanja hiki kinapokea watalii zaidi ya milioni moja na wameendelea kuhamia hapa kwa sababu ni kiwanja salama,” amesema Myeya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uongozaji Ndege kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Florah Alphonce amesema hali ya usalama katika uwanja huo ni shwari na imeimarishwa.

“Wiki hii tunahamasisha tamaduni za kiusalama kwenye viwanja vyetu vya ndege. Mategemeo yetu ni kuhamasisha wadau wa anga na wale wanaozunguka eneo hili kujua ni nini tunapaswa kufanya ili kuimarisha usalama,” amesema Alphonce.

Related Posts