Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania inatarajia kuwazawadia wateja na mawakala wake katika msimu huu wa sikukuu.
Zawadi hizo zitatolewa kupitia promosheni maalumu iliyozinduliwa leo Desemba 17,2024 ijulikanayo kama Airtel Santa Mizawadi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa promosheni hiyo makao makuu ya Airtel Tanzania jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano, Jackson Mmbando, amesema inalenga kuwashukuru wateja na mawakala waaminifu na wanaoendelea kutumia Airtel katika msimu wote wa sikukuu.
“Airtel Santa Mizawadi ni promosheni kabambe ambayo itawapa washindi fursa ya kuondoka na zawadi mbalimbali ikiwemo pocket WiFi, simu janja, pikipiki, luninga na fedha taslim hadi shilingi milioni moja.
“Kupitia Promosheni ya Airtel Santa Mizawadi tunasambaza upendo na kunogesha sikukuu kwa wateja na mawakala wetu ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio yetu,” amesema Mmbando.
Mmbando amesema Airtel inaendelea kujidhatiti kutoa huduma za kipekee katika msimu wa sikukuu huku akidokeza kuwa kila muamala unaofanyika unatoa nafasi kwa wateja au mawakala kujishindia zawadi zitakazoboresha maisha yao.
Kwa upande wake Meneja Huduma kwa Wateja, Celine Njuju, amesema; “Airtel tunawathamini sana wateja wetu, tusingefika hapa tulipo leo bila ya wateja na mawakala wetu, Airtel Santa Mizawadi ni promosheni kabambe kwa kuwa itanogesha balozi wetu.
“Mtamuona Mr SANTA wetu akitembelea baadhi ya mitaa yetu kuhakikisha wateja na mawakala wanapata pia zawadi za papo kwa hapo, ikiwa utabahatika kukutana naye basi nakuahidi atanogesha msimu wako wa sikukuu vizuri ufurahie wewe na wapendwa wako,” amesema Njuju.
Amesema washindi wa Airtel Santa Mizawadi watapatikana kupitia droo zitakazochezwa kila wiki mara moja ambapo wote watapigiwa simu kupitia namba maalumu ya Airtel 100.
“Jinsi ya kushiriki na kujishindia Airtel Santa Mizawadi, ikiwa wewe ni wakala wa Airtel unatakiwa kufanya miamala ya kuweka na kutoa fedha, pia ili mteja aweze kuingia kwenye droo anatakiwa kufanya miamala kama vile kununua bando, kutuma fedha, kutoa fedha, kulipa bili, kufanya miamala ya kibenki, kutuma au kupokea fedha nje ya nchi, kununua muda wa maongezi au vifurushi kupitia 14999#, 15060#, au kwa kutumia ‘My Airtel App’,” amesema.