MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Alassane Diao, amerejea kwenye kikosi hicho kwa kufunga bao baada ya kukosekana uwanjani kwa takribani miezi tisa.
Diao raia wa Senegal, tangu Machi 2024 alipofanyiwa upasuaji wa goti kufuatia majeraha yake ya Anterior Cruciate Ligament (ACL), hakuonekana uwanjani mpaka leo Desemba 17, 2024 alipoingia dakika ya 81 kuchukua nafasi ya Jibril Sillah wakati Azam ikishinda 2-0 dhidi ya Fountain Gate.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Diao alifunga bao hilo dakika ya 90+1 kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na Cheikh Sidibe.
Kabla ya bao hilo, Jibril Sillah alifunga kipindi cha kwanza dakika ya 31 kwa asisti ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye sasa amefikisha saba kwenye ligi msimu huu na kuendelea kuongoza.
Ushindi huo unaifanya Azam kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 33 ikicheza mechi 15 ikishinda 10, sare tatu na kupoteza mbili, ikifunga mabao 22 na kuruhusu saba ikiwa juu ya Singida Black Stars yenye pointi 30 na mechi 14.
Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na mechi 11 na pointi 28 wakati Yanga ni ya nne, imeshuka dimbani mara 11 ikikusanya pointi 27.