Katavi. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi, kimewaonya makada wake walioanza harakati hizo mapema kinyume na taratibu za chama hicho.
Kwa mujibu wa duru za ndani ya chama hicho, Mkoa wa Katavi wenye majimbo matano ya uchaguzi, wamejitokeza zaidi ya makada 30 ambao wameanza kupitapita majimboni, jambo linalowapa presha wabunge walio madarakani.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 17, 2024 kuhusu jambo hilo, Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Idd Kimanta amebainisha kuwa tayari uongozi wa chama hicho umepata taarifa hizo sambamba na orodha ya baadhi ya wanachama ambao wameanza kujipitisha.
Amesisitiza kwamba muda wa wao kufanya hivyo haujafika, hivyo wanakiuka kanuni na maadili ya chama hicho, jambo ambalo hawatalivumilia, na watawachukulia hatua za kinidhamu wote watakaothibitika kufanya hivyo.
‘’Tayari tumepata orodha ya majina ya wanachama wetu ambao wameanza kujipitisha kwenye majimbo na kata kutangaza nia ya kuomba nafasi za ubunge na udiwani, naomba niwaambie kuwa muda bado haujafika kuanza hizo harakati.”
“Bado tuna madiwani kwenye kata na wabunge wetu katika majimbo yote matano ambao wanaendelea kutekeleza ilani ya chama na kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo,” amesema.
Amebainisha kuwa chama kiko makini na kinaendelea kufuatilia mienendo ya wanachama hao kwa karibu na endapo kitajiridhisha, kitachukua hatua kwa mujibu wa taratibu za chama na wasije kulaumu kwa kuwa zinaeleweka na lazima zifuatwe.
Kimanta amewataka wanachama hao kufuata taratibu kwa kusubiri wakati rasmi wa michakato ya uchaguzi ndani ya chama, waanze harakati hizo kwani kuanza kupita kwa wananchi wakati huu ni kuwakosea heshima wabunge na madiwani ambao wapo kisheria hadi mwaka 2025.
Amesema pamoja na kuwepo kwa vuguvugu na joto la uchaguzi mkuu mwaka 2025 ni ishara ya kukua kwa demokrasia ndani ya CCM, na kutoa nafasi kwa wanachama kuonyesha nia hiyo kwa kufuata taratibu za chama na siyo mihemko ya kisiasa.
Katika hatua nyingine amekanusha vikali tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa baadhi ya viongozi wa CCM, mkoani humo kuleta wagombea kwa ajili ya kuomba nafasi za udiwani na ubunge kwenye kata na majimbo ya uchaguzi katika mkoa huo.
“Hakuna kiongozi yeyote wa chama anayeweza kuleta mgombea kwa ajili ya uchaguzi ujao, kuna taarifa hizo kwamba fulani analeta wagombea, naomba niwaambie wanaCCM wenzangu, jambo hilo halipo ni uzushi tu,” amesema.