DC Kilakala: Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala amesema mtu yeyote atakayekamatwa akihujumu miundombinu ya reli, barabara, umeme ama maji hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Kilakala ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Desemba 17, 2024, kufuatia taarifa za kuongezeka kwa matukio ya wizi wa miundombinu, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa.

“Serikali imewekeza fedha nyingi kupitia kodi za wananchi katika ujenzi wa miundombinu hii, lakini kuna watu wachache wasioitakia mema nchi na wasiojali masilahi ya Taifa wanafanya wizi huu. Serikali haitakubali hali hii iendelee.” Hatutawaacha salama, tutawachukulia hatua kali,” amesema Kilakala.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limewakamata watu sita, wakiwamo watatu wanaoshukiwa kuhujumu miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na miundombinu ya kilimo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Desemba 3, 2024 katika Kijiji cha Mandera, Wilaya ya Mvomero, wakihusishwa na wizi wa rola tano za nyaya za umeme zenye thamani ya Sh57 milioni.

“Baada ya tukio hilo, timu ya makachero wetu ilifanya ufuatiliaji wa kina na kufanikiwa kukamata nyaya hizo Desemba 6, mwaka huu katika Mtaa wa Boma, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam,” amesema Kamanda Mkama.

Amebainisha kuwa waliokamatwa ni Dismas Petro (28), fundi umeme mkazi wa Dar es Salaam; Alawi Evodius (32), mfanyabiashara mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam na Muhoza Bombo (40), dalali mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi limewakamata watu watatu wa jamii ya kifugaji kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya kilimo katika Kitongoji cha Msimba, Kijiji cha Ilonga, Wilaya ya Kilosa.

Kamanda Mkama amesema tukio hilo lilitokea Desemba 6, mwaka huu na watuhumiwa hao wanatuhumiwa kukata uzio wa Shamba la Taifa la Mbegu la Msimba kwa kutumia mkasi na kuingiza mifugo yao, hali iliyosababisha uharibifu mkubwa.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Miligo Komiyani (26), Moringe Rombo (30) na Hamis Lambaigwa (27), wote wakazi wa Kilosa na ni wa jamii ya wafugaji.

Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa matukio hayo unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Related Posts