Madai ya serikali ya Kongo ni kuwa kampuni hiyo ya kiteknolojia inatumia madini yanayotokana na migogoro nchini mwake katika uzalishaji wa bidhaa zake.
Mawakili wa kimataifa wanaoiwakilisha Kongo, wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kampuni ya Apple hutumia madini yaliyoibwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kusafirishwa kimagendo kupitia minyororo na ugavi wa kimataifa, hali ambayo inaiweka kampuni hiyo kuwa mhusika katika uhalifu unaofanyika Congo.
Kulingana na malamishi yaliyowasilishwa katika ofisi ya muendesha mashtaka mjini Paris Ufaransa na vilevile katika ofisi ya uchunguzi nchini Ubelgiji, Congo inazituhumu kampuni tanzu za Apple France, Apple Retail France na Apple Retail Belgium kwa makosa mbalimbali
Miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na kuficha uhalifu wa kivita, utapeli wa madini yaliyopatikana katika maeneo ya migogoro, kushughulikia bidhaa za magendo, na kushiriki vitendo vya udanganyifu vya kibiashara.
Machafuko ya DRC yachochea magendo ya madini
Akitaja ripoti za Umoja wa Mataifa kuhusu machafuko ya mashariki mwa Kongo, wakili Christophe Marchand kutoka Ubelgiji amesema ni wazi kwamba kampuni tanzu za Apple, nchini Ufaransa na Ubelgiji zinafahamu fika kwamba madini kwenye minyororo yao ya uzalishaji yanatokana na matendo yaliyo kinyume cha sheria.
Unaweza pia kusoma: Waasi wa M23 wauteka mji wa madini wa Rubaya nchini Kongo
Marchand amesema Ubelgiji ilikuwa na wajibu wa kuchukua hatua kwa sababu uporaji wa malighafi ya Kongo ulianza karne ya 19 wakati wa utawala wa kikoloni wa Mfalme Leopold wa Pili. Kwa hivyo ni wajibu wa Ubelgiji kuisaidia Kongo katika juhudi zake kusaka haki mahakamani kukomesha wizi huo.
Ufaransa na Ubelgiji zilichaguliwa kwa sababu ya maoni kwamba zinatilia msisitizo mkubwa, uwajibikaji wa mashirika. Mahakama katika mataifa yote mawili zitaamua kuchunguza malalamiko zaidi na kuleta mashtaka ya jinai.
Kongo ni chanzo kikuu cha madini kama bati, tantalum na tungsten, maarufu kama 3T yanayotumika kwenye kompyuta na simu za mkononi. Lakini baadhi ya migodi kunakochimbwa madini hayo, inasimamiwa na vikundi vyenye silaha vinavyohusika na mauaji ya raia, ubakaji, uporaji na aina mbalimbali za uhalifu. Hayo ni kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa na makundi ya haki za binadamu.
Apple yajitetea dhidi ya magendo ya madini
Kampuni ya Apple hainunui madini hayo moja kwa moja kutoka yanakochimbwa. Kampuni hiyo imesema huwa inawachunguza wasambazaji wa madini, huchapisha ripoti za chunguzi zao na pia huyafadhili mashirika yanayojizatiti kuboresha maadili katika uchimbaji na uuzaji wa madini.
Unaweza kusoma pia: Je Ulaya ina nafasi gani katika soko la Cobalt ya Congo?
Tangu miaka ya 1990, maeneo ya uchimbaji madini mashariki mwa DRC yameharibiwa kufuatia mawimbi ya mapigano kati ya makundi yenye silaha. Baadhi ya makundi hayo huungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, na vilevile jeshi la Kongo.
Rwanda hukanusha madai ya kunufaika na magendo ya madini ya DRC. Kutokana na migogoro hiyo, mamilioni ya raia wameuawa na kuyakimbia makaazi yao.
Ushindani wa madini, ni moja ya vichocheo vikuu vya migogoro huku makundi yenye silaha yakijiendeleza na kununua silaha kutokana na mapato ya mauzo ya madini nje ya Kongo.
Robert Amsterdam, wakili kutoka Marekani amesema malalamishi ya jinai yaliyowasilishwa Ufaransa na Ubelgiji, ndiyo ya kwanza ya serikali ya Congo dhidi ya kampuni kubwa ya kiteknolojia na ameeleza kuwa huo ni mwanzo tu.
(Reuters)