Familia ya Ulomi yakubali ndugu yao amefariki kwa ajali

Dar es Salaam. Hatimaye familia ya mfanyabishara Daisle Ulomi aliyefariki na mwili wake kukutwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, imesema kuwa ndugu yao ni kweli alifariki kwa ajali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 17, 2024, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema ajali hiyo ilitokea Ubungo Extenal Makuburi mchana na walitokea wasamaria wema waliosaidia kumpeleka mwili huo hospitali.

“Tukio lile lilitokea mchana kweupe na wasamaria wema waliojitolea wenye ubinadamu na utu licha ya kwamba ilikuwa ajali mbaya ambayo kama ukiona ule mwili utajua ni kwa nini hata ndugu walipopita mochwari walishindwa kumtambua,” amesema.

Akizungumza na wanahabari leo Mikocheni ambako familia imeweka msiba, msemaji wa familia hiyo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko amesema baada ya mwili kupatikana Mwananyala walipigiwa simu kisha baadhi ya ndugu walienda kuangalia na kuutambua.

“Tupo kwenye taratibu za maombolezo ya kwenda kumstiri ndugu yetu ambaye alipata ajali Desemba 11, 2024 saa 7:55 mchana katika maeneo ya Gereji akiwa anatokea Barabara ya Mandela baada ya kutokea ajali watu wema walimpeleka kituo cha afya Makuburi,” amesema.

Amesema taratibu za mazishi zinaendelea na wanatarajia kuuaga mwili wa marehemu Alhamisi Desemba 19, 2024 katika Kanisa la Kijitonyama na atakwenda kuzikwa Mkoa wa Kilimanjaro.

“Salamu zote zitatolewa pale na utaratibu wote wa kumuaga utakuwa pale na baada ya hapo tutaanza safari ya kuusafirisha mwili hadi Kilimanjaro,” amesema.  


Polisi yafafanua kilichomuua Ulomi

Bomboko amekiri taarifa za kupotea hadi kuja kuonekana ndugu yao zimekuwa na mkanganyiko, huku akieleza wakati anaondoka kwenye shughuli zake alienda kufuata mzigo wake Bandari Kavu.

“Akiwa njiani alifikwa na umauti kwa ajali na taarifa zilitolewa na Jeshi la Polisi na ndio uhalisia, awali kama familia tulitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yetu na tulipata ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Polisi na tumeridhika na taarifa yao na kilichobaki kwenda kuupumzisha mwili,” amesema.

Amesema wameridhika na taarifa ya jeshi hilo baada ya kuona picha za mwili hivyo taarifa yao inaonyesha uhalisia.

“Hatupo kwenye fikra kwamba alipotezwa, tumeridhika na tumepokea, kimsingi hakuwa mtu mwenye ugomvi na watu hakuwa mwanaharakati na wala si mwanasiasa na hakuwa mfanyabiashara mkubwa kihivyo na hakuwa na changamoto ya kuweza kusema amepotezwa,” amesema.  

Related Posts