DAR City imemaliza nafasi ya pili kwenye michuano ya Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, lakini gumzo kubwa lilikuwa ni Hasheem Thabeet kutokana na mavitu yake.
Kwenye mashindano hayo, Hasheem alionyesha kiwango kizuri ikiwamo kupokonya mipira kwa kiwango kikubwa.
Pia nyota huyo wa zamani wa Oklahoma City Thunder ya Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) ndiye aliyeongoza kwa kuwekewa ulinzi na wapinzani.
Umbo lake na nguvu ni moja ya mambo yaliyombeba na kuwa tishio kwa wapinzani na alichukua mipira ‘rebound’ na kuzuia ‘blocks’.
Katika michuano hiyo, Remesh ya Burundi iliibuka mabingwa baada ya kushinda michezo yake yote mitano, ikifuatiwa na Dar City (TZ), KPA (Kenya), Equity (Kenya), ABC (Tanzania) na Hippos (Burundi).
Dar City katika michezo yake, ilishinda dhidi ya Equity Bank kwa pointi 84-64, KPA 69-65, ABC 66-58, Hippos 84-40, kabla ya kufungwa na Remesh kwa pointi 77-58.
Baada ya fainali hizo, Remesh , Dar City na KPA zilikabidhiwa vikombe na medali, huku Thabeet akikabidhiwa cheti maalumu cha ushiriki wake.
Zawadi zingine zilizotolewa ni za mchezaji bora, Nathaniel Brownlee (Dar City) na mfungaji bora, Jonas Mushi wa ABC.
Zawadi nyingine zilizotolewa ni kwa Gilbert Nijimber ‘Point Gurd’ (Remesha), Salim Kisiiu ‘Power Forward’ (KPA) Landry Ndikumana ‘Centre’ (Remesha).