Jela miaka 30 kwa kosa la kumbaka mwanafunzi

 Kwimba. Mkazi wa Kijiji cha Nkalalo kilichopo Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Nicholas James (21) amehukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa kidato cha nne (19) katika Shule ya Sekondari Taro.

Hukumu hiyo imetolewa Desemba 16, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kwimba, John Jagadi baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi watano akiwemo mwanafunzi aliyetendewa kitendo hicho, kwenye kesi ya jinai namba 22882 ya mwaka 2024.

Akitoa ushahidi mahakamani hapo, mwanafunzi huyo ambaye alikuwa ni shahidi wa kwanza, amesema alibakwa akiwa njiani kufuata maji kisimani.

“Nilikuwa nakwenda kisimani kuchota maji, nikakutana na mtuhumiwa akanikamata na kunivutia kichakani huku akinitishia kunichoma kisu nikipiga kelele na kunivua chupi na kuanza kunibaka,” amesema.

Hakimu Jagadi, baada ya kusikiliza mashahidi wa pande zote na upande wa Jamhuri kutoa ushahidi wa kuthibitisha mtuhumiwa kutenda kosa hilo pasi shaka, alimtia hatiani na kumpa nafasi ya kuomba kwa nini asichukuliwe hatua kali za sheria.

Akijitetea,  James aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa shetani alimpitia lakini pia anategemewa na wazazi.

Mahakama, baada ya kusikiliza maombi yake, iliyatupilia mbali na kuuomba upande wa mashitaka kumbukumbu ya makosa yake ya nyuma.

Mwendesha mashitaka, Juma Kiparo aliiambia Mahakama hakuna makosa ya nyuma na kuiomba itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa vijana kama huyo kuvizia wanafunzi wanaotumwa na wazazi wao kuteka maji visimani.

Mahakama ilimuhukumu kifungo cha  miaka 30 jela ili liwe fundisho kwa wengine ikisema rufaa iko wazi ndani ya siku 30.

Awali, Kiparo akimsomea hati ya shitaka hilo Agosti 14, 2024, aliieleza Mahakama kuwa huko katika Kijiji cha Nkalalo saa 4 asubuhi, mtuhumiwa alimkamata  mwanafunzi huyo, kumvua nguo za ndani kisha kumbaka kinyume na kifungu cha Sheria 130 (1)(2) na kifungu 131(1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ya sheria kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Related Posts