NYOTA wa Simba, Kibu Denis ‘Mkandaji’ ambaye aliwafanya wachezaji na maofisa wa CS Sfaxien kurusha ngumi kwa mwamuzi Andoftra Revolla Rakotojuana, amefichua mazito yaliyowabeba katika mchezo wao wa Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kibu ndiye aliyefunga mabao yote mawili dakika ya saba na 90+8 katika ushindi wa 2-1 uliowaweka Simba katika nafasi nzuri ya kuendelea kupambania kutinga robo fainali ya michuano hiyo baada ya kufikisha pointi sita sawa na Bravos na Constantine.
“Tulijua kuwa hatukuwa kwenye hali nzuri baada ya kufungwa mapema,” alisema Kibu akirejea kwenye dakika ya tatu, wakati ambapo CS Sfaxien walifunga bao la kuongoza kupitia kwa Hazem Haj Hassen.
“Lakini tulijua kuwa mchezo haukuwa umeisha na tulikuwa na nafasi ya kurudi nyuma na kupigana. Sisi kama wachezaji, hatukukubali kushindwa.”
Katika dakika ya saba, Kibu alijibu mapigo kwa kufunga bao la kusawazisha akitumia kichwa akimalizia pigo la frii-kiki kutoka kwa Jean Charles Ahoua. Bao hilo lilikuwa ni faraja kubwa kwa wachezaji na mashabiki wa Simba, kwani lilirudisha matumaini kwa timu hiyo na kwenda mapumziko ikiwa sare ya 1-1.
“Kichwa changu kilikuwa kimejaa mawazo ya jinsi ya kuisaidia timu yangu,” alisema Kibu akielezea namna alivyotupia bao hilo.
Simba ilitengeneza nafasi nyingi katika kipindi cha pili lakini ilikosa kuzitumia vyema. Kuhusu hilo, Kibu alisema kila mchezaji alijua jukumu lake na alijitahidi kuwa sehemu ya ushindi huo.
“Tulijua kuwa hatukuwa tumeisha. Tuna wachezaji wazuri hivyo tulipambana kila mtu kwa nafasi yake,” alibainisha Kibu huku akikiri kwamba mchezo huo haukuwa rahisi.
“Ushindi hauji kwa urahisi. Tulijua kuwa tunahitaji kupigania hadi mwisho, hata kama tumekosa nafasi nyingi. Lakini ukweli ni kwamba kila mmoja alijitahidi kupigania hadi mwisho na hii ndio siri yetu,” alisema Kibu, ambaye alifunga bao la pili la ushindi dakika ya 90+8, kwa kichwa akimalizia krosi ndefu kutoka kwa Yusuf Kagoma.
“Wakati wa kuongeza dakika, wengi walikuwa wanajiuliza kama tungeweza kufunga bao la pili. Lakini sisi tulijua kuwa kama tungeendelea kupigana, tungeweza kufikia lengo letu,” alisema Kibu akizungumzia jinsi walivyokuwa wanapigana hadi dakika za mwisho.
“Kila mchezaji alijua kuwa kazi haikuwa imeisha hadi filimbi ya mwisho inalia. Nilijua kuwa nafasi yangu itakuja, na nilijitahidi kuimaliza kazi,” alihitimisha Kibu ambaye kwenye ligi hajafunga bao kwa takribani siku 407 tangu mara ya mwisho afunge Novemba 5, 2023 Simba ilipofungwa 5-1 na Yanga lakini kimataifa msimu huu anayo matatu. Moja alifunga Simba iliposhinda 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli kwenye mtoano.
Kwa ushindi huu, Simba ilifikisha pointi sita katika Kundi A, ikiwa imecheza mechi tatu, na kuendelea kuwa na matumaini makubwa ya kufuzu kwa hatua ya mtoano.
Mchezo ujao Januari 5, 2025 Simba itakwenda Tunisia kucheza na CS Sfaxien ambayo imepoteza mechi zote tatu za kwanza, baada ya hapo Januari 12 itakuwa Angola kukabiliana na Bravos kisha itarejea Dar Januari 19 kumalizana na CS Constantine.