MSHIKEMSHIKE wa Ligi Kuu Bara unaendelea leo Jumanne kwa kuchezwa mechi mbili zitakazozikutanisha timu ngumu katika kuwania pointi za kibabe.
Saa 10:00 jioni, Tabora United iliyopo nafasi ya 5 na pointi 24, itaikaribisha Coastal Union iliyopo nafasi ya 9 baada ya kukusanya pointi 16, mechi hii itapigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo mkoani Tabora.
Tabora United ambao ni wenyeji wa mchezo huo, wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata matokeo mazuri katika mechi iliyopita dhidi ya Azam FC kwa kushinda mabao 2-1, wakati Coastal Union ikitoka kupoteza 3-2 dhidi ya Fountain Gate.
Kabla ya mchezo wa leo, Tabora United ina rekodi ya kucheza mechi sita mfululizo za ligi msimu huu bila ya kupoteza ambapo imetoka sare moja dhidi ya Singida Black Stars (2-2) huku ikishinda tano dhidi ya Pamba Jiji (1-0), Mashujaa (1-0), Yanga (3-1), KMC (2-0) na Azam (2-1). Mara ya mwisho kupoteza ilikuwa Oktoba 18 mwaka huu ilipofungwa 4-2 na JKT Tanzania.
Kwenye uwanja wa nyumbani, Tabora United mechi tano za mwisho imepoteza moja dhidi ya Fountain Gate (3-1), huku ikishinda tatu na sare moja.
Hii inaonyesha kwamba Tabora nyumbani haipo kinyonge hivyo Coastal Union ambayo haijashinda mechi yoyote ugenini kati ya tano za mwisho zaidi ya sare tatu na kupoteza mbili ina kazi ya ziada ya kufanya kuhakikisha inapata matokeo mazuri.
Mchezo mwingine unatarajiwa kupigwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. Wenyeji Azam watapambana na Fountain Gate.
Azam wametoka kupoteza mchezo wa ugenini, huku Fountain Gate wakishinda nyumbani, hivyo kazi itakuwa si nyepesi kwani wenyeji wanataka kuendelea kufanya vizuri kupambania nafasi yao kileleni wakati wageni wao wakitengeneza mazingira ya kuisaka nne bora.
Kwa sasa Azam inaongoza ligi ikiwa na pointi 30 baada ya kucheza mechi 14, leo utakuwa ni mchezo wa kuhitimisha mzunguko wa kwanza huku chini yao Simba (28) na Yanga (27) zikiwakimbiza kwa ukaribu ambapo wakongwe hao wamecheza michezo 11 kila mmoja.
Fountain Gate iliyopo nafasi ya sita na pointi 20 ikishuka dimbani mara 13, bado inaonekana kuwa na tatizo la kuruhusu mabao mengi (23) licha ya kwamba yenyewe nayo inafunga ikiwa na idadi kama hiyo.
Kocha wa Coastal Union, Juma Mwambusi alisema: “Hautakuwa mchezo rahisi, tunazihitaji pointi tatu muhimu baada ya kutoka kupoteza, tumesahau matokeo yaliyopita, tunajipanga kuhakikisha tunaonyesha ubora na kupata pointi tatu.”
Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi alisema hautakuwa mchezo rahisi lakini hawawezi kurudia makosa kama waliyoyafanya mchezo uliopita hivyo wanatarajia matokeo mazuri.