Pwani. Ukinzani wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya 1999 na Sheria ya Misitu Namba 14 ya 2002 vimetajwa kuwa chanzo cha uharibifu wa misitu ya mikoko, ambapo mpaka mwaka 2020 zaidi ya hekta 7,000 zimefyekwa kati ya hekta 53,255 zilizopo katika Delta ya Kibiti Rufiji kwa ajili ya kilimo, Mwananchi limeelezwa.
Hayo yanatokea licha ya ukweli kwamba Tafiti ya Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa (UNU) ya mwaka 2020 na Taasisi ya Mazingira na Usalama wa Binadamu inasema misitu ya mikoko ina ufanisi wa juu zaidi katika kuondoa hewa ya ukaa kwenye mazingira kuliko misitu ya aina nyingine. Pia iliongeza zaidi ya robo ya mikoko imepotea duniani katika miaka 40 iliyopita.
Hili pekee linaifanya misitu hiyo kuwa sehemu muhimu ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kupunguza ongezeko la joto duniani.
Kwa Tanzania kutokana na uharibifu huo, Serikali inaandaa mpango mkakati wa kitaifa wa usimamizi wa mikoko Tanzania unaotarajiwa kuzinduliwa Julai 2025. Delta ya Mto Rufiji ndio inayoongoza kuwa na mikoko mingi Afrika Mashariki, ikifuatiwa Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi yenye hekta 23,422.
Akizungumza na Mwananchi kwa niaba ya Kamishina wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo kuhusu hatua zinazochukuliwa, Ofisa Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Frank Sima anasema tatizo la uharibifu wa mikoko ni kubwa kiasi cha kuhitaji juhudi jumuishi.
“Hifadhi ya Misitu ya Mikoko eneo la Delta ni hekta 53,255 lakini kupitia taarifa mbalimbali inaonekana kupungua kwa kiwango ambacho kwa kweli kinahitaji hatua za makusudi za Serikali,” anasema.
Anasema uharibifu huo umechangiwa na kilimo kisicho endelevu, uvamizi wa malisho ya mifugo na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha kuongezeka kwa kimo cha ujazo wa maji ya bahari.
“Madhara yake ni pamoja na kuongezeka kwa nguvu ya mawimbi ya bahari yanasababisha mmomonyoko wa fukwe ambayo huleta mchanga zaidi ufukweni na kusababisha mikoko kufa kama inavyoonekana kwenye baadhi ya visiwa vya Delta ya Mto Rufiji Wilaya ya Kibiti.
“Taarifa za kiutafuti na mojawapo ni taarifa ya Serikali ya NAFORMA (Mkakati wa Ufuatiliaji wa rasilimali za Misiti Tanzania Bara) ya mwaka 2015 inaonyesha ukubwa wa maeneo ya Hifadhi za Mikoko Tanzania.
“Aidha, katika tathmini mpya ya rasilimali za mikoko katika Delta ya Mto Rufiji iliyofanyika mwaka 2020 inaonyesha maeneo yaliyokatwa kwa ajili ya kilimo cha mpunga hadi kufikia 2020 yalikuwa ni hekta 7,000 lakini taarifa zaidi zinaonyesha eneo hilo limeongezeka zaidi,” anasema.
Anakitaja kilimo cha mpunga kushamiri katika eneo hilo na hivyo kuathiri misitu ya mikoko.
“Maji baridi ya Mto Rufiji yakifika eneo ambalo mto huo unamwaga maji yake Bahari ya Hindi hilo la kukutana huwa yanainuka juu na kusambaa katika eneo kubwa la zaidi ya hekta 10,000 hapo ndipo wananchi wanatumia eneo hilo kulima mpunga,” anasema.
Wakati sheria ya misitu ikisisitiza uhifadhi, sheria ya ardhi za vijiji inaruhusu wanavijiji kufungua mashamba katika ardhi iliyotengwa kulingana na mfumo wa matumizi bora ya ardhi.
Katika hilo, Sima anaeleza historia ya operesheni vijiji vya ujamaa ya mwaka 1971.
“Serikali ilianzisha na moja kati ya maeneo ambavyo vijiji vilianzishwa ilikuwa pamoja na visiwa vidogo vya Delta ya Rufiji.
“Kuna visiwa vidogo 43 na ndani ya hifadhi ya mikoko vipo 24 ambavyo ndani yake kuna vijiji 19 vilivyoandikishwa na maeneo wanayolima mpunga kwenye meneo ya vijiji vyao, kwa hiyo kuna mkanganyiko wa sheria,” anasema.
Anafafanua kuwa awali miaka ya 1960 kabla hata vijiji vya ujamaa havijaanza wanajamii katika maeneo hayo walikuwa wanavitumia visiwa hivyo kwa shughuli za uvuvi na kilimo kilikuwa nje ya misitu ya mikoko.
“Walikuwa wanalima nje ya eneo la Delta kwenye vijiji vya Kikale, Mtunda A na B, Twsalie, Msala, Maparoni vyote vya Wilaya ya Kibiti na hata leo kuna mabaki ya matrekta yaliyokuwa yakitumika,” anasema.
Akijadili suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG), Charles Meshack anasema sheria ya ardhi za vijiji, kutunza msitu ni hiari ya kijiji.
“Tatizo ni kwamba hata wakitunza msitu, wakati wa kuuvuna, wataomba vibali TFS ambayo ndio inachukua mapato yote, lakini kama kijiji kikigeuza msitu kuwa mashamba, sheria ya ardhi za vijiji inatambua kwamba wameendeleza ardhi,” anasema.
Wananchi na TFS lugha gongana
Wakati TFS ikiendelea na urejelezaji wa mikoko kwenye maeneo yaliyoharibiwa kwa kilimo, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Nyamisati, wanasema ndio maeneo wanayotegemea kwa kilimo.
Sakina Anthony, mkulima wa mpunga katika kijiji hicho anasema urejelezaji wa mikoko umewaathiri katika kilimo chao.
“Mipunga bado tunapanda humo humo wanamopanda mikoko, lakini tatizo mikoko inapandwa karibu karibu, mpunga unashindwa kustawi. Anasema kwa sasa wanazuiwa kuongeza mashamba huku maeneo wanayolima wakiongezwa mikoko.
“Sisi sio wavamizi wa mikoko, ni mikoko ndio imetukuta na ndio maana tunapambana tu kulima hivyo hivyo ukipata kiroba kimoja cha kula na watoto unashukuru,” anasema.
Fatuma Ally, anasema wakati mashamba yao yakipandwa mikoko, wao hawashirikishwi.
“Mtu anakuja kupata miti kwenye shamba langu bila kuniambia. Tunaomba Serikali iweke mpango wa kutusaidia,” anasema. Maoni hayo pia yametolewa na Husna Moshi aliyeomba Serikali iwapatie maeneo mbadala ya kulima.
Ofisa Mhifadhi wa TFS, Sima anasema kutokana na uharibifu, Serikali imekuja na mpango mkakati wa kitaifa wa usimamizi wa mikoko Tanzania unaotarajiwa kuzinduliwa Julai 26, 2025 ambayo ni siku ya mikoko duniani.
“Mkakati huo utataja namna ya kuondoa mkanganyiko wa kisheria, kikanuni na mikanganyiko ya kimaamuzi ya uhifadhi wa mikoko Tanzania,” anasema.
Pia anataja mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa sera ya misitu wa miaka 10 kuanzia mwaka 2021 hadi 2030 unaotekelezwa na idara ya misitu na nyuki ukilenga kuboresha utekelezaji wa Sera ya Misitu ya 1998.
“Ukisoma ibara ya 4 (2) na (7) ya mkakati huo, kutokana na uharibifu huo kuwa mkubwa, Serikali imeruhusu wadau wa kitaifa na kimataifa kushirikiana na Serikali za halmashauri za wilaya kukabiliana na uharibifu huo,” anasema.
Anataja pia visababishi vingine yakiwemo mahitaji ya kila siku, kilimo cha mpunga katika Delta ya Kibiti, uanzishwaji wa mashamba ya chumvi usiofuata taratibu. “Hutokea wale walioanzisha mashamba ya chumvi huwa wanatamani tena kuongeza mashamba hayo na kukata mikoko,” anasema.
Kibano wavunaji wa mikoko
Kwa mujibu wa Sima, uvunaji wa mikoko unatajwa katika kanuni na maelekezo yaliyotajwa kwenye mpango wa uhifadhi wa misitu ya mikoko, ikiwemo misitu ya Delta ya Rufiji.
“Mpango wa kwanza ulikuwa mwaka 1991 na ukapitiwa upya mwaka 2021 na ukaanza kutumika Julai 2021 na utatumika hadio 2025.
“Mpango umeainisha kanda nne ambazo ni kanda ya ulinzi wa misitiu ya hifadhi, kanda ya pili ni ya uvunaji, kanda ya tatu ni ya urejeshaji wa mikoko na kanda ya nne ni ya uwekezaji,” anasema.
Katika kanda ya pili ya uvunaji, anasema TFS iliweka mpango wa uvunaji wa mikoko katika Wilaya ya Kibiti na iliainisha aina tatu za mikoko inayotakiwa kuvunwa, ambazo ni Mkaka, Mkandaa na tatu ni Mchu.
Anataja vipimo vinavyoruhusiwa kuvunwa kuwa ni nguzo zilizo katika madaraja manne ambayo ni zenye unene kati ya sentimita 15 mpaka 20, pili sentimita 10 hadi 15 na tatu sentimita 15 kurudi nyuma kidogo na nne nguzo zenye unene wa sentimita 10.
“Ikitokea mtu anakiuka vipimo hivyo anakuwa anaharibu mikoko,” anasema.
Anataja pia mwongozo wa matumizi ya mazao ya mikoko, na kama wanajamii wana mahitaji yasiyo ya kibiashara wanaruhusiwa, ikiwamo kutengenezea majahazi au mitumbwi, mpini, matendegu ya vitanda, mpini wa shoka au jembe, Serikali imeweka utaratibu.
“Serikali pia imevipa fursa vijiji vinavyozunguka misitu ya mikoko Tanzania nzima (Bara) kuwa na fursa ya kuandaa sheria zao ndogo, ili kusimamia misitu katika vijiji vyao na kukusanya tozo zilizo chini ya halmashauri,” anasema.
Kutokana na ukiukwaji wa sheria na taratibu zilizowekwa, Sima anasema mpaka sasa kuna kesi tano zinaendelea kwenye Mahakama tofauti nchini za watu waliokamatwa wakikata na kusafirisha magogo ya mikoko kinyume cha sheria.
Itaendelea kesho. Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917