Munthary akoleza vita na Camara, Diarra

KIPA wa Mashujaa, Patrick Munthary amekoleza vita ya kuwania Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufikisha ‘clean sheet’ nane, hivyo kutangaza vita na washindani wake, Moussa Camara wa Simba na Djigui Diarra kutoka Yanga.

Munthary amefikisha ‘clean sheet’ hizo nane katika michezo 12 kati ya 14 ya timu hiyo akizidiwa moja na kinara, Camara mwenye tisa, huku Diarra akiwa nazo saba, jambo linaloamsha ushindani zaidi ikiwa mzunguko wa kwanza unakwenda tamati.

Hatua hiyo kwa Munthary ya kuendelea kukoleza vita kwa makipa wa Simba na Yanga imejiri baada ya Mashujaa kulazimishwa suluhu na maafande wenzao wa JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar esa Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Munthary alisema siri kubwa ya kiwango chake kwa sasa ni kutokana na ushirikiano baina yake na wachezaji wenzake, huku akiweka wazi anachokiangalia ni kuendelea kuipambania timu hiyo ili kufanya vizuri.

“Jambo la kwanza ninaloliangalia ni kuona timu yetu inafanya vizuri katika kila mashindano tunayoshiriki msimu huu, hayo mambo mengine yangu binafsi yatafuata kwa sababu mchezaji yeyote ni lazima awe na malengo aliyojiwekea,” alisema.

Related Posts